KANISA MORAVIAN KUJENGA SHULE YA WASICHANA JIJINI DAR ES SALAAM.
Kanisa la Moravian Kinondoni,moja ya majengo ya kisasa ya kanisa hilo nchini. |
Kanisa la Moravian Jimbo la Mashariki, Wilaya ya Kaskazini limeanza kuendesha harambee ya kutafuta Sh milioni 400 za kujenga Shule ya Sekondari ya Wasichana jijini Dar es Salaam.
Katika hatua za awali, tayari kanisa hilo limenunua ekari 100 katika eneo la Kibamba mpakani na Kiluvya, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo. Ikikamilika, huenda zaidi ya wanafunzi wa kike 60 kwa awamu ya kwanza, watapata nafasi.
Hatua hii ni ya kupongezwa kwa kuwa ni wazi watakaofaidika na shule hiyo, si tu watoto wa washirika wa kanisa hilo, bali Watanzania kwa ujumla na hivyo kuwezesha kutengeneza wasomi zaidi katika vizazi vijavyo nchini.
Harambee ya kwanza ya ujenzi huo unaoleta historia ya shule ya kwanza ya kanisa hilo Wilaya ya Kaskazini, ilifanyika wiki kadhaa zilizopita katika ukumbi wa Kanisa la Moravian la Mabibo na lengo lilikuwa ni kuchangisha Sh milioni 60 za awali ili kuwezesha hatua za ujenzi kuanza.
Ujenzi huo kwa mujibu wa viongozi wa kanisa hilo, unafanyika kwa awamu katika eneo la ekari 50 linalojumuisha pia ujenzi wa hospitali baada ya shule kukamilika. Eneo lililobaki litakodishwa kwa wawekezaji ili fedha zitakazopatikana, zimalize kulipia eneo zima la ekari 100 ambalo hivi sasa wanalipa kwa awamu.
Harambee iliyofanyika Mabibo ilihusisha watu mbalimbali, wakiwemo wageni waalikwa, wachungaji na washirika wa kanisa hilo wa Wilaya hiyo ya Kaskazini. Kikanisa Wilaya hiyo inajumuisha Wilaya ya kiserikali ya Kinondoni na Mkoa wa Pwani. Katika harambee hiyo, zilipatikana Sh milioni 30 ikiwa ni nusu ya kiwango kilicholengwa kukusanywa. Mwenyekiti wa Wilaya hiyo, Mchungaji Alinanuswe Mwakilema, anatumia fursa hiyo kueleza wananchi kuwa lengo la ujenzi huo ni kuendeleza juhudi za serikali katika kupambana na adui ujinga na umasikini kwa kuwezesha kufungua akili za watoto wa Kitanzania.
“Mipango ni mingi lakini kwa mwanzo tumeanza na ujenzi wa shule hii ya wasichana, ni imani yetu kuwa ujenzi utawagusa wananchi wote wenye mapenzi mema kwa kuwa tunawalenga wote kunufaika na shule hii,” anasema Mchungaji Mwakilema. Anasema kwa muda mrefu kanisa hilo lililo chini ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) limekuwa likishughulika na masuala ya kiroho zaidi ya kimwili hivyo kusababishwa kuachwa mbali kimaendeleo na makanisa wanayoshirikiana nayo (ya CCT), ikiwemo Katoliki na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).
“Huo ndio ukweli, lakini pia tulijikita zaidi kutoa huduma za kiroho vijijini na si mijini, hii imetuweka mbali na maendeleo mengine, sasa tumedhamiria kutekeleza wajibu huu mijini pia, tunaomba wananchi wenye nia njema watuunge mkono,” anasema Mchungaji Mwakilema. Mwenyekiti huyo anaeleza “Tumeanza harambee hii ya kwanza ya kukusanya shilingi milioni 60, lengo ni kupata Sh milioni 400 lakini tunaanza na hii ili kuanza utekelezaji wa awali. Lengo kuu la kujenga shule hiyo ni kutambua umuhimu wa watoto wa kike kwa ustawi wa kanisa na taifa letu”.
Anasema kanisa linaamini katika uwezo mkubwa walionao watoto wa kike tofauti na dhana iliyojengeka katika jamii kwamba watoto wa kike ni dhaifu ikilinganishwa na watoto wa kiume. “Tulikaa kama kanisa na kufikiri pia kuwa, kuliko kuanza na shule mchanganyiko, tuanze kwanza na sekondari ya wasichana, tumeamua hivi kwa kuwa kuna ushahidi mkubwa katika jamii hivi sasa kwamba wasichana na wanawake, ni kiini cha maendeleo ya jamii,” anasema Mchungaji huyo.
Anafafanua kuwa, kwa miaka mingi jamii imekuwa ikiwathamini watoto wa kike kutokana na utamaduni uliojengeka tangu awali kuwa mtoto wa kike yupo kwa ajili ya kufanya kazi za nyumbani na kusubiri kuolewa na wa kiume ndiye anayetakiwa kusoma, jambo lililosababisha kwa kiasi kikubwa watoto wa kike kutojiamini kielimu. Mwenyekiti huyo anasema shule hiyo, itazingatia misingi ya maadili ya Kitanzania na itaajiri walimu wenye uzoefu mkubwa katika kufundisha hivyo malengo ni kushika nafasi za juu za ushindi kwa ngazi ya kitaifa hapo masomo yatakapoanza.
Anasema hilo ni miongoni mwa dhamira kuu ya kutekeleza lengo la muda mrefu la kujenga shule hiyo ili kuudhihirisha ulimwengu kuwa wasichana wanaweza kuleta mapinduzi kupitia elimu. Kauli hiyo inaungwa mkono na Mchungaji Emaus Mwamakula, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Harambee akinukuu maandiko ya Kitabu Kitakatifu cha Biblia yanayosema ‘mwanangu ishike sana elimu, wala usimwache aende zake’, anasisitiza kuwa elimu ni ufunguo wa maisha ya kiroho na kimwili.
Anasema maendeleo ya jamii yoyote, yanategemea maisha ya mtu yanayohusisha mwili na roho, hivyo ni wajibu wa kanisa kushirikiana na serikali kuhakikisha kuwa jamii inanufaika kiroho na kimwili. Mchungaji Mwamakula anasema sababu hiyo na nyingine ndiyo imewagusa kutekeleza mpango huo wa kujenga shule ya wasichana Kibamba na kueleza kuwa harambee zitafanyika kwenye makanisa ya Moravian yaliyo chini ya usimamizi wa Wilaya ya Kaskazini.
Akifafanua namna nyingine wanaoitumia kukusanya fedha za ujenzi mbali na harambee, Mchungaji Mwamakula anasema kanisa limetengeneza kadi maalumu kwa ajili ya washirika wa kanisa hilo wanaotoa kuanzia Sh 2,000 hadi zaidi ya Sh 300,000. Viongozi hao waamini kuwa kwa kila Mtanzania mpenda maendeleo, atajitokeza kushirikiana nao katika kufanikisha ujenzi huo. Anaeleza kuwa zitakapopatikana Sh milioni 60 za awali, hatua ya kuweka msingi wa shule itaanza mara moja. “Hatuwezi kusema kama ni leo au kesho kwa maana ya mwaka huu au mwakani tutaanza kujenga, ila tukipata fedha hata kesho, tutaanza kujenga maana kinachosubirisha ni fedha, tumekubaliana kwamba zikipatikama shilingi milioni sitini, ujenzi wa msingi uanze wakati michango ikiendelea,” anasema Mchungaji Mwamakula.
WIMBO ''MAFARAKANO'' WA KWAYA YA EFATHA KUTOKA KARIAKOO MORAVIAN.
Comments