RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

KIJANA ALIYENUSURIKA KUTOLEWA KAFARA MGODINI AJISALIMISHA KWENYE KONGAMANO LA MAOMBI


Mchungaji Florian Katunzi akiongoza maombi wakati wa kongamano aliloliandaa na kanisa analosimamia la EAGT City Centre jijini Dar es salaam.

Kongamano la siku nane la maombi na maombezi lililomalizikia hivi karibuni Jijini Dar es Salaam, limewaponya na kuwafungua watu wengi waliokuwa wakiteswa na Shetani kwa kuwatoa katika ‘majeneza’  ya magonjwa na matatizo sugu yaliyokuwa yakiwasumbua, akiwemo kijana Rashid Selemani (25) aliyenusurika kutolewa kafara  na wachimbaji madini  Wilayani Nachingwea mkoani Lindi.

Umati  wa watu ulishuhudia kijana huyo akitambaa kama nyoka wakati akiombewa uponyaji, ambapo baada ya kuponywa alitoa ushuhuda wake jinsi yeye na wenzake  kumi walivyoshauriwa kwenda kwa mganga wa kienyeji na kuchemshwa katika sufuria ili kufanikisha upatikanaji wa madini.
Alisema  yeye na wenzake hao walikuwa wachimbaji madini ya dhahabu katika mgodi mmoja mkoani humo, ambapo ‘mabosi’ wao waliwashauri kwenda kwa mganga wa kienyeji ili kupata dawa, bila kujua nia ya mabosi hao  ilikuwa kuwatoa kafara.

“Tupofika kwa mganga tulilazwa katika chumba chenye joka kubwa lililotuchanja chale tatu katika miguu ya kulia  na baadaye tulichemshwa katika sufuria kubwa la maji ya moto na kupatiwa dawa”, alisema kijana Sulemani na kuongeza kuwa baada ya kurudi katika mgodi wa dhahabu, walijikuta wakipata ajali mbaya ya kuangukiwa na kifusi.

Alisema anamshukuru Mungu kwamba wafanyakazi wenzao waliwaokoa yeye na wenzake wawili waliokuwa wamefukiwa pamoja, ambapo katika harakati za uokoaji alijeruhiwa mguuni na kumsababishia jeraha linalomfanya atembee akichechemea.

Kijana  Selemani ambaye wakati akiombewa uponyaji alikuwa akipiga  kelele na kutembea kama nyoka kutokana na mapepo yaliyokuwa yamempagaa, alisema baada ya kunusurika kutolewa kafara  alikimbilia Jijini Dar es Salaam maeneo ya Mwembeyanga.
Alisema siku moja alikutana na wanawake waliokuwa wakisukana na akawauliza  sehemu lililopo kanisa la kilokole.

Kijana Selemani alisema wanawake hao  walimwelekeza kwenda kwenye viwanja vya Sabasaba na ndipo alipofika katika Ukumbi wa PTA na kushiriki katika kongamano la Maombi na mombezi lililokuwa likiendeshwa na Mchungaji Florian Katunzi wa Kanisa la EAGT City Centre.

Uponyaji wa kijana Selemani na ushuhuda wake ni sehemu ya miujiza mikuu ya uponyaji iliyorindima katika siku nane za kongamano hilo lililowatoa wengi kutoka katika ‘majeneza’ ya mateso ya shetani.
Katika siku ya mwisho ya kongamano hilo lililovuta maelfu ya watu katika ukumbi wa PTA ulioko katika viwanja vya Maonesho ya Kimataifa ya Biashara vya Mwalimu Nyerere maarufu kama Sabasaba, ujumbe uliotolewa na Mchungaji Katunzi ulihusiana na Injili ya Luka 7:11-17.

Injili hiyo inazungumzia jinsi Yesu Kristo Bwana wa uhai alivyomfufua mtoto wa mama mjane aliyekuwa amekufa katika mji na Naini, kwa kuwaambia watu waliokuwa wamebeba jeneza  wakielekea kumzika waliweke chini,  kisha akaligusa na kuiambia maiti iamke na ikatii mara moja.
Ujumbe wa leo ni maombi ndani mwa maombi, ambapo kila pando asilolipanda Baba Yetu wa Mbinguni litang’olewa”, alisisitiza Mchungaji Katunzi katika mahubiri yake.
Mchungaji Katunzi aliendesha maombezi mazito ya kuwatoa watu kutoka katika majeneza ya utasa, magonjwa, mapepo, umasikini, kudharauliwa, matatizo ya ndoa, majini, wachawi na matatizo mengine mengi.

Wengi walioondolewa katika majeneza hayo kupitia maombezi hayo, walidondoshwa na nguvu za  Mungu na kukimbizwa katika chumba maalum  kupatiwa huduma za kiroho na timu maalum ya maombezi ya watendakazi wa Kanisa la EAGT City Centre.
Mara baada ya kumalizika kwa kongamano hilo la Maombi na Maombezi, Mchungaji Katunzi aliliambia gazeti Msemakweli kuwa yuko katika maandalizi ya kongamamo jingine la siku nne la Maombi na Maombezi litakalofahamika kama Anza mwaka na Bwana 2013.

Alisema kongamano hilo litaanza Desemba 29, 2012  na kumalizika Junuari 1, 2013 katika ukumbi wa PTA, likiwa maalum kwa ajili ya kuwaingiza Watanzania mwaka 2013 kwa ujumbe wa baraka za kifamilia, utakaojikita zaidi katika masuala ya uchumi na elimu.

Limeandika Msemakweli.

Comments