| Anthony Alli Ramadhani akirejea kifungu kutoka kichwani mwake wakati wa ibada |
Ni siku ya Alhamisi wiki iliyopita ambapo ofisi za Gazeti Msemakweli
zinapata Mgeni wa aina yake ambaye aliacha simulizi ambayo ni vigumu
kuaminika, lakini ukweli unabaki pale pale kwamba Mgeni huyo ana uwezo
wa ajabu wa kukariri Maandiko Matakatifu yaliyomo katika vitabu
mbalimbali vya Biblia, na kuyasoma neno kwa neno kutoka kichwani mwake
bila kukosea neno hata moja.
Kijana huyo aliyejitambulisha kwa jina la Athony Alli Ramadhani (36)
aliyeokoka mwaka 1996 katika Kanisa la Pentekoste Tabora mjini ni zao
linalotokana na mama mkristo na baba Mwislamu, ambao hata hivyo
walitengana wakati kijana huyo akiwa bado mdogo.
Athony ambaye kwa sasa anaishi Jijini Dar es Salaam na ni mshirika wa
Kanisa la kilokole la Ufufuo na Uzima lililoko Kawe, alilifika katika
ofisi za Gazeti hili akiwa ni Biblia yake iliyochakaa ikionesha kwamba
imekuwa ikinasomwa sana.
Katika mahojiano na Gazeti hili alisema kuwa nia yake ni kuhakikisha
kuwa anaikariri Biblia nzima kuanzia kitabu cha Mwanzo hadi Ufunuo wa
Yohana na akaonesha kwa vitendo kudhihirisha kiu yake hiyo, kwa kusoma
sura 15 za kitabu cha Mwanzo bila kukosea neno.
Aidha kijana Athony alisema tayari amekariri sura nyingi za vitabu vya
Zaburi na Hesabu lakini kiu yake ni kuimaliza Biblia nzima, kwani uwezo
anao isipokuwa kinachomkwamisha ni muda na shughuli nyingi za kutafuata
maisha bila kupata muda mzuri wa kupumzia na kusoma Biblia yake.
“Baada ya kuokoka nilikuwa na kiu sana ya kumjua Mungu na kumtafuta
Mungu kupitia neno lake, ndipo siku moja nikiwa nimelala Mungu alijibu
maombi yangu na kunionesha maono yaliyonitaka nisome kwa bidii neno
lake”,alisema Kijana Athony ambaye wakati wa mahojiano na agazeti hili,
alikuwa akipokea simu nyingi kutoka kwa watu waliokuwa wakiulizia sehemu
yalipo Maandiko fulani Matakati katika Biblia Takatifu na yeye kuwajibu
haraka papo kwa hapo bila kukosea.
“Nakumbuka siku moja mchana nilisikia sauti ambayo naamini ni ya Mungu
ikinitaka nikalale. Nilitii na ndipo nikiwa usingizini nililetewa kitabu
mbele yangu na tazama nilishuhudia maandishi ya moto yakipita katika
kurasa zake. Baadaye nikasikia sauti ikiniambia kwamba napaswa kukariri
maandiko hayo kisha ndoto hiyo ikakoma nikaamka”, alisema kijana
Anthony.
Alisema tangu wakati huo alianza kusoma Biblia na kujikuta kila akisoma
maandiko yote anayosoma yanakaa kichwani na kwamba kamwe hayasauliki.
“Hali ndivyo ilivyo ndugu Mwandishi. Nitaka niikariri Biblia nzima ila
kwa sasa nafanya kazi ya bodaboda na nyingine ambazo zinachukuwa muda
wangu mwingi. Nataka sana nipate mtu wa kunifadhili ili nikasome niwe
mchungaji kabisa kwa vile najua Mungu ameshaniita, ila tatizo ni
fedha.Akitokea mtu akanifadhili nitafurahi sana”, alisema Kijana huyo
ambaye katika kanisa lake analosali anafahamika kama Mchungaji mshauri
kutokana na huduma ya kuwapa ushauri wa kiroho Wakristo wapya na
wenyeji.
Alisema elimu yake ni ya darasa la nne inayomuwezesha kusoma vyema
Biblia ya Kiswahili na kuandika, lakini angefurahi zaidi kama angepata
ufadhili pia wa kusomweshwa lugha ya Kiingereza ili aikariri Biblia
nzima ya Kiingereza kama anavyofanya kwa Biblia ya Kiswahili.
Gazeti hili lilitaka kujua namna watu wanavyouchukulia uwezo wake mkubwa
wa kukariri maandiko ya Biblia ambapo alisema anamshukuru Mungu kwamba
Mchungaji wake Josephat Gwajima anamkubali na kumwelewa na kwamba siku
moja alishawahi kumtambulisha mbele ya kanisa na akamuombea na kumtaka
asonge mbele na kazi ya Injili.
“Najua watu wengine wanakataa kipaji nilichopewa na Mungu na wanasema ni
nguvu za giza zinazoniongoza kitu ambacho sio cha kweli. Tazama
Mwandishi, Shetani hawezi kujifitini kiasi hiki kwa kunipa uwezo huu ili
nieneze Injili ya Yesu Kristo. Ninachojua mimi ni kwamba aliyenipa
uwezo huu ni Mungu mwenyewe kupitia Roho Mtakatifu kwa ajili ya kuujenga
ufalme wake na sio wa Shetani”, alisema kijana Athony.
Limeandika Gazeti Msemakweli.
Comments