
Askofu mkuu wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk
Valentino Mokiwa ameshindwa kutetea nafasi yake ya uaskofu mkuu wa
kanisa hilo Tanzania baada ya kushindwa na Dk Jacobo Chimeledya (56) wa
Jimbo la Mpwapwa.
Askofu Chimeledya ambaye anakuwa kiongozi wa sita kushika wadhifa huo
nchini, aliibuka mshindi baada ya jina lake kupenya katika hatua tatu za
kura.
Akitangaza matokeo hayo jana jioni, Katibu Mkuu wa Anglikana, Dk Dickson
Chilongani alisema kanisa hilo halina utaratibu wa kutangaza kura
zilizopigwa lakini akathibitisha kuwa Askofu Chimeledya ndiye mshindi.
Dk Chilongani alisema kuchaguliwa kwa Askofu Chimeledya ni utaratibu wa
kanisa hilo ambalo hufanya uchaguzi kila baada ya miaka mitano.
Uchaguzi huo ulianza kwa ibada iliyoongozwa na Askofu wa Dayosisi ya
Dodoma, Godfrey Mhogolo na baada ya hapo, Msajili wa kanisa hilo,
Profesa Palamagamba Kabudi alitangaza utaratibu wa uchaguzi.
Chilongani alisema wajumbe 129 walihudhuria mkutano huo kati ya wajumbe 140 waliotarajiwa.
“Kwa kawaida katika uchaguzi, askofu yeyote mwenye umri chini ya miaka
60 huwa anaweza kuwa mgombea na katika uchaguzi huo, maaskofu 21
walikuwa na sifa za kugombea,” alisema.
Dk Chilongani alisema Askofu Chimeledya alizaliwa mwaka 1957 na alisoma
stashahada ya theolojia katika Chuo cha St. Philipo kilichopo Kongwa,
Dodoma.
“Baadaye alikwenda Kenya na kuchukua shahada ya masomo ya dini katika
Chuo cha St. Paul kabla ya kwenda kusomea shahada ya uzamili katika
theolojia Marekani,” alisema.
Askofu Chimeledya aliteuliwa kuwa Askofu Mwandamizi wa Jimbo la Mpwapwa chini Askofu Simon Chiwanga mwaka 2007.
Baada ya Askofu Chiwanga kustaafu Dk Chimeledya aliteuliwa kuwa askofu wa dayosisi hiyo.
Alisema askofu huyo mpya atawekwa wakfu mwishoni mwa Mei mwaka huu
katika ibada itakayofanyika katika Kanisa Kuu la mjini Dodoma.
Limeandika : Mwananchi
Comments