RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

KANUNI 10 ZA MBOLEA ZA MANENO YA KUTIA MOYO KWA WANANDOA


Na mchungaji Peter Mitimingi

1. Wanawake wengi wananjaa ya kusikia maneno mazuri kutoka kwa waume zao. Lakini wanaume ni wagumu sana kusifia wake zao wengi hupenda kusifia wanawake wengine kule nje lakini sio mke wake. Jambo hilo huwakwaza sana wanawake.

2. Usiwe mtu wa kukatisha tamaa katika kila jambo kwa kutoa kauli mbaya na ngumu kwa mwenzi wako. Unamkatisha tamaa mkeo kwamba hawezi kitu au unamkatisha tamaa mumeo kwamba hanalolote ni sawa na mvaa suruali tu. Huko siko kujenge ndoa imara.

3. Hata kama jambo ni gumu kiasi gani usionyeshe hali ya kukatisha tamaa na kumvunja moyo. Tumia mbinu kuinua kiwango cha moyo cha mwenzi wako na kubadilisha hali madhaifu yake kuwa mafanikio. Mtie moyo mwezi wako aendelee mbele na sio kukata tamaa na kumrudisha nyuma.

4. Kabla hujatamka neno hakikisha ni maneno yaliyopata kibali kabla ya kutamkwa. Jiwekee chujio mdomoni kabla ya kutamka. Chuja maneno yote yaliyobeba sumu inayojeruhi moyo wa mwenzi wako kabla hujatamka. Midomo yako iteme asali kwa mwenzi wako sio iteme sumu.

5. Mwenzi wako ni rafiki yako, rafiki mara zote huambiwa maneno mazuri. Usitumie maneno ya ukali kwa mwezi wako mpaka akawa na hofu kukushirikisha kitu kwa kuhofia majibu makali atakayo yapokea kutoka kwako.

6. Usitumie maneno ya kashfa kwa mwenzi wako. Usitumie maneno ya kumdharilisha hata kama kweli kakosea. Hatakama unataka kueleza tatizo la mwenzi wako tumia maneno mazuri kumueleza na kwa wakati muafaka.

7. Mwenzi wako akifanya jambo zuri jitahidi kumpongeza, nakuonyesha kwamba kweli kafanya jambo zuri. Usichukulie kwamba ni jambo zuri na likaishia moyoni mwako. Usijikaushe liseme wazi. (speak it out) Akipika vizuri mpongeze, akivaa vizuri mpongeze kama ni mume akifanya vizuri kazini mpongeze.

8. Mpongeze mwenzi wako mbele za watu wengine, watoto wenu, wazazi wake marafiki zako au marafiki zake hiyo inajenga ujasiri mkubwa na kujiamini sana kwa mwanandoa anayepongezwa mbela za watu wengine n.k

9. Mpongeze mwenzi wako mbele za watu wanao mchukia au kumdharau sana. (Maadui zake). Hiyo itamjengea kujithamini na kupata uhakika wa kujiona kuwa yeye tayari ni mshindi pia itamuondolea hofu na kujidharau.

10. Maneno yanaumba. Ukimtamkia mwenzi wako maneno mabaya basi ujue hayo mabaya yatamfuata. Ukimtamkia mwenzi wako maneo mazuri basi ujue mambo mazuri yatamfuata.

Comments