Nyota wa nyimbo za Injili Bongo, Bahati Lusako Bukuku ameumia mgongo na maeneo kadhaa ya mwili (nusu kifo) kiasi cha kushindwa kukaa, kusimama wala kutembea kufuatia ajali mbaya ya gari iliyotokea kwenye eneo la Ranchi ya Narco wilayani Kongwa, Dodoma saa tisa usiku wa kuamkia Jumamosi.
Katika ajali hiyo ambayo Bahati alikuwa akienda Kahama, Shinyanga kwenye mkutano wa Injili, dereva wa gari alilokuwa akisafiria aina ya Toyota Nadia lenye namba za usajili IT 7945, Edison Mwakabungu ‘Eddy’ (31) aliumia sana kwenye vidole vya miguu na hawezi kutembea.
Wengine waliokuwemo kwenye ajali hiyo ni wacheza shoo wa Bahati, Frank Muha (20) na mwenzake ambaye jina lake halikupatikana mara moja.
Alfajiri ya juzi, mwandishi wa habari hizi alimpigia simu Bahati na kuongea naye kuhusu ajali hiyo ambapo huku akisikika kama anayepata taabu kwa maumivu, alisema:
“Ni kweli tumepata ajali, nimeumia mgongoni, dereva ameumia mguu. Namshukuru Mungu. Sijui nini kilitokea, nilishtukia kuona gari kubwa mbele yetu likituvaa, mara nikashtukia tuko porini. Lakini kabla ya safari Dar tulifanya maombi makubwa, najua Mungu ametunusuru na kifo kibaya,” alisema Bahati.
Kumbukumbu zinaonesha kuwa hii si mara ya kwanza kuripotiwa kwa ajali za magari mkoani Dodoma zikiwahusisha watu wa tasnia Injili Bongo.
Aprili, mwaka huu, Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotion, Alex Msama alipata ajali mbaya ya gari kwa kugongana na mwendesha bodaboda. Ajali hiyo ilitokea maeneo ya Ipagala Mwisho, kilomita chache kabla ya kufika mjini Dodoma. Msama alikuwa kwenye gari lake aina ya Toyota Mark II GX 100.
Comments