RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

MIMBA YENYE HATARI YA KUHARIBIKA



Mwandishi: Dk. A. Mandai

WIKI iliyopita nilieleza tatizo la mimba kutoka mara kwa mara na nikaahidi leo kuelezea mimba zenye hatari ya kuharibika.

Mimba yenye hatari ya kuharibika ni hali inayojitokeza kwa mjamzito kutoka damu ukeni wakati wa wiki za mwanzo za ujauzito mpaka wiki ya 20.

Hali hii huashiria dalili ya mimba kutaka kuharibika au kutoka, ingawa ujauzito unaweza kuendelea mpaka kujifungua na kitaalam huitwa

Threatened Abortion. Asilimia 20 mpaka 30 ya wajawazito hutokwa na damu wakati wa ujauzito, hasa miezi ya kwanza wengi wao bila mimba kuharibika. Mara nyingi dalili inayojitokeza ni kutokwa damu ukeni.

Inaweza kuwa kama vitone kwenye nguo za ndani au damu kabisa kutoka. Mwanamke anaweza akapata na maumivu chini ya kitovu au kiunoni.

Yapo baadhi ya mambo ambayo huleta hatari ya mimba kuharibika, mambo hayo ni kuumia tumboni, maambukizi ya magonjwa, kupata mimba ukiwa na zaidi ya miaka 35 na matumizi ya kahawa kwa wingi mwanamke akiwa mjamzito.

Unapopata dalili tulizoeleza hapa ni muhimu uwahi hospitali kwa uchunguzi zaidi. Uchunguzi hufanyika na mimba yenye hatari ya kuharibika, shingo ya uzazi huwa bado imefunga vizuri.

Vipimo kama Ultrasound ya tumbo, kipimo cha ujauzito cha mkojo hufanyika ili kuthibitisha uwezekano wa mimba kuendelea au vipimo vya kutazama kundi na wingi wa damu.

TIBA YAKE

Mjamzito anatakiwa kupumzika bila kufanya shughuli yoyote, hii ni sehemu muhimu ya matibabau ya tatizo hili na inasaidia kupunguza hatari ya mimba kuharibika.

Katika kipindi hiki mjamzito anatakiwa kuzingatia yafuatayo; kama alikuwa anafanya mazoezi, anatakiwa asitishe pia asitishe kufanya mapenzi na mwenzi wake.

Mjamzito anatakiwa kupunguza unywaji wa vinywaji vyenye caffeine kama kahawa au chai, anashauriwa kufuatilia kliniki ya ujauzito na vipimo kama atakavyoelekezwa na kituo chake cha kliniki.