RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

SOMO: UNDANI WA MAOMBI ( 10-11) - MCHUNGAJI MADUMLA


Bwana Yesu asifiwe


Ndani yangu nasikia,leo tuanze kwa kukumbushana kule tulikoanza safari yetu ya somo hili zuri na adimu,ili uweze kuelewa ni wapi tulikotoka,na ni wapi tupo na ni wapi tunakoelekea.

Somo hili tuliligawa katika vipenge 11,navyo ni kama ifuatavyo;

01.Nini maana ya maombi?

02.Kwa nini tunaomba.?

03.Aina za maombi.

04.Jinsi ya kuomba vizuri.

05. Mifano ya waombaji waliofanikiwa.

06.Mazingira yafaayo katika maombi

07.Mazingira yasiyofaa katika maombi.

08.Mkao mzuri wa maombi/Mikao katika maombi.

09.Sababu ya kutojibiwa maombi yako.

10.Faida za maombi.

11.Mathara ya kuishi bila maombi.

~Mpaka sasa,bado tupo katika kipengele namba 3 tukijifunza aina za maombi;Tumeshamaliza kujifunza aina tano za maombi,leo tunajifunza kwa ufupi aina ya sita ya maombi kwa mujibu wa mpangilio wangu. Nayo ni;

(VI) MAOMBI YA NADHIRI.

Neno nadhiri ni kiapo cha maneno yanayowekwa baina ya pande mbili,upande wa anaweka nadhiri na upande wa Mungu wake. Hivyo;Nadhiri ni ahadi ya maneno maalumu juu ya kutimiliza jambo au kitu fulani baada ya kujibiwa au kutendewa na yule unayemuomba.

Yule anaweka nadhiri ni yule aliyeomba akitumaini kupokea kwa kutoa kitu fulani au jambo fulani (baada ya kujibiwa) Aina hii ya maombi,ni hatari sana. Na hatuwashauri watu wawe wanaomba kinadhiri katika kila ombi kwa sababu ikiwa utaomba omba kinadhiri na hujafanikiwa kuziondoa hizo nadhili ni dhambi.

Nini chanzo cha maombi haya?

Chanzo chake cha maombi ya nadhiri ni pale mwombaji aliyeomba jambo kwa muda mrefu pasipo kulipata,sasa anaamua kuweka nadhiri kwamba akilipata nae atatoa kitu au jambo kwa Mungu wake. Wengine huweka nadhiri za kuwatoa watoto wao kwa Bwana kama ilivyokuwa kwa Hana alivyoweka nadhiri yake kwa mwanae Samweli;

“ Naye huyo mwanamke alikuwa na uchungu rohoni mwake, akamwomba BWANA akalia sana.Akaweka nadhiri, akasema, Ee BWANA wa majeshi, ikiwa wewe utaliangalia teso la mjakazi wako, na kunikumbuka, wala usinisahau mimi mjakazi wako, na kunipa mimi mjakazi wako mtoto mume, ndipo mimi nitakapompa BWANA huyo mtoto siku zote za maisha yake, wala wembe hautamfikilia kichwani kamwe.” 1 Samweli 1:10-11

Je maombi haya yapo mpaka leo? 

Ndio,maombi haya yapo mpaka hivi leo. Tumeshuhudia mara nyingi watu wakiweka nadhiri kwa Mungu tuwapo kanisani,na kwa sababu hii;watu wengi wamefungwa kwa sababu wengine wameshindwa kuzitoa au kuzitimiliza. Biblia inasema; 


“ Utakapoweka nadhiri kwa BWANA, Mungu wako, usiwe mlegevu katika kuiondoa; kwa kuwa BWANA, Mungu wako, hataacha kuitaka kwako; nayo hivi itakuwa dhambi kwako.” Kumb.23:21

Kumbe ni dhambi kwa yule aliyeweka nadhiri kisha hakuiondoa. Ni heri usingeliweka maana haitakuwa dhambi kwako( Kumb.23:22). Watu wengi leo wameingia katika dhambi hii pasipo kujua,na wengine wameingia wakijua kwamba ni dhambi.

Angalia mfano huu halisi ;katika changizo kanisani; utakuta mtu yupo mbele za madhabahu ya Bwana kisha anaahidi mchango wa kiasi kikubwa cha pesa ambacho hana uwezo nacho,ili mradi watu wamuone,wamsifie lakini ukweli ni kwamba watu wengi wa namna hii wanakuwa hawatoi hizo pesa,au la kama wakitoa basi itachukua muda mrefu sana mpaka akamilishe mchango wake.

Sasa hii ni dhambi sana,kwa nini usiweke ahadi nzuri ya kawaida ambayo roho yako inaridhika,kusudi usije ukaingia katika dhambi? Lakini wengi walioweka ahadi za pesa mbele za Bwana,si kana kwamba hawapati pesa hizo ili wazitoe nadhiri zao la hasha! Mungu ni mwaminifu Yeye huwapa pesa hizo ili waweze kutimiliza ahadi zao.

Tatizo linakuja pale,mtu anapopata pesa hizo,hula zote.Anajikuta akizila kwa matumizi mengine ambayo ni kinyume kabisa na kusudio la pesa hizo. Mfano; Umeweka ahadi ya pesa ya tshs 200,000/= alafu kwa kuwa Mungu ni mwaminifu,akaanza kukupa kidogo kidogo. Leo akakupa Tshs 50,000,/= ikapita wiki mbili,akakupa tshs 130,000/= then baada ya muda fulani hivi akakumalizia tshs 20,000/= . 

Sasa angalia,pale alipoanza kukupa elfu hamsini,wewe ukamega hiyo pesa,ukajinunulia viatu. Baadae ulipopata pesa ingine,ukaona gauni zuri,ukanunua,mara ukachukua pesa hiyo hiyo ukaenda saloni kusuka N.K( na kwa wanaume ni vivyo hivyo.) Gafla ukajikuta umekosa pesa ya kulipa ahadi yako,nayo ahadi sasa hugeuka kuwa dhambi.

Ifike wakati sasa tuwe makini na semi zetu haswa tuwapo mbele za Bwana. Tuache roho ya mazoea mbele Bwana,ni dhambi mbaya sana. 

Wapo watu,wala hawajalogwa,wala hakuna uchawi,wala si shetani bali wanateseka kwa sababu hawajaziondoa nadhiri zao. Hivyo hujikuta wakistrago sana katika maisha yao kwa maana wamejisahau kuziondoa ahadi na nadhiri zao walizoziweka.

Maombi haya hayafanywi kiholela olela tu!,ni lazima uzingatie yafuatayo;

(a) Uwe na akili timamu juu ya kile unachotaka kuweka nadhiri.

(b) Umuombe Roho mtakatifu akupe amani juu ya nadhiri utakayoiweka. La! Kama umekosa amani usiweke nadhiri kabisa.

(c)Ukiwa una mwenzi wako wa ndoa,au mtu wa karibu yako,basi umshirikishe ili wote wawili mkumbuke nadhiri yenu au yako.

(d)Ni lazima uandike nadhiri yako,kwa sababu usije ukaisahau na ikawa ni dhambi.

(e)Uwe mwaminifu kutoa kile ulichomuahidi Mungu. N.K

Je ufanye nini ikiwa ulimwekea Bwana ahadi na umeshindwa kuitoa?

~Jambo la kwanza kabisa,ni kufanya toba kwa damu ya Yesu….

(VII) MAOMBI YA MAPATANO/UMOJA.

Hii ni aina ya saba ya maombi katika mpangilio niliokupa. Maombi haya ni muhimu sana kwa sababu yamebeba nguvu kubwa tena ya kupekee kuliko aina ya maombi yoyote ile. Waswahili husema“ umoja una nguvu…” kati ya jambo ambalo Bwana Yesu analisisitiza sana ni suala la umoja. Yoh.17:21

Umoja ni Roho ya Kristo;kwa maana ni vema tukawa pamoja kwa umoja (Zab. 133:1) sisi ambao ni ndugu katika Kristo Yesu. Neno “umoja” kama lilivyotumika katika Zab.hii linawakilisha “umoja wa roho” yaani ni sawa na kusema “Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza,Ndugu wakae pamoja katika hali ya mwili na, kwa umoja wa roho.” Sababu waweza ukawa pamoja na mtu,lakini papo hapo msiwe kwa umoja. 

Na hii ndio hatari kubwa leo,wakristo wengi tupo pamoja lakini si kwa umoja,yaani ,kweli tunaonekana ni wakristo sababu tunaitwa jina moja,lakini hatupo na umoja wa roho,na ndio maana utakuta huyu kamsema yule na yule kamsema huyu hali sote tu wakristo tuliokoka.

Kumbe kazi tuliyonayo ilikuwa ni kuungana pamoja kwa umoja,tupambane na adui yetu shetani,lakini hali haiko hivyo,leo;mchungaji husimama muda mrefu akimsema mchungaji mwenzake badala ya kufundisha neno la Mungu.

Maombi ya mapatano ni pale ambapo waombaji hupatana kwa kwa nia moja katika yale wanayoyaomba. Mfano waombaji wanaweza wakawa na ajenda ya kuombea taifa kwa siku tatu,hivyo hukutana pamoja kwa maombi wakisimamia ajenda hiyo hiyo kwa wote bila kutengana.

Maombi ya mapatano hayakuanzia leo,yalikuwepo zamani hata tangu kipindi cha akina Danieli. Tuangalie biblia inatuelezaje juu ya mfano wa maombi haya;

“ Ndipo Danieli akaenda nyumbani kwake, akawapasha habari kina Hanania, na Mishaeli, na Azaria wenzake;ili waombe rehema kwa Mungu wa mbinguni kwa habari ya siri hiyo, ili kwamba Danieli na wenzake wasiangamizwe pamoja na wenye hekima wa Babeli.” Danieli 2:17-18

Andiko hili linatupa picha ya kwamba akina Danieli walinia mamoja katika maombi yao. Walifanya maombi ya mapatano ambayo Mungu alionekana akimjibu Danieli. Si kana kwamba Danieli alikuwa hawezi kuomba yeye mwenyewe,la! bali alikuwa anajua nini faida ya maombi ya umoja.

Je kwa nini maombi ya mapatano? Kwani Mungu hakusikii pale uombapo peke yako?

Tukumbuke jambo hili,Mungu huangalia moyo wa mwombaji na wala haangalii idadi ya waombaji. Hii ikiwa na maana kwamba Bwana Mungu husikia maombi yako binafsi ukiomba katika moyo.

Pia,kumbuka kwamba imo nguvu kubwa pale mfanyapo maombi ya mapatano ikiwa wote mpo rohoni na mpo na muambatano wa roho;yaani kile ulichonacho kinashabiana na mwenzako au wenzako (lakini isiwe wengi,mara nyingi ni wachache). Tazama vile Bwana Yesu akisema;

“Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni.“Mathayo 18:19

MAMBO YA KUZINGATIA KATIKA MAOMBI HAYA;

(a) Usafi wa kiroho kwa wale watakao patana katika maombi~ kama utapatana na mwezako msimame katika nia moja ya maombi,basi hakikisha kwanza wewe uwe na usafi wa rohoni pia mwanzako lazima awe na usafi wa rohoni la sivyo ni bora msipatane. 

Mfano;Chukulia mpo katika mfungo wa siku tatu wa maombi wewe na mwenzako mkiombea ajenda fulani kwa kumaanisha lakini papo hapo mwenzako akakosa uaminifu akawa ni muongo akijifanya anafunga huku anakula kinyemela nyemela pale mnapokuwa mmeachana kila mmoja anarudi kwake. Hapo maombi yenu ni sawa na bure kwa sababu mmoja amekosa uaminifu katika patano lenu.

(b) Hakikisha wewe huna kinyongo na mtu yeyote yule(hujamshikilia mtu yoyote yule,umesamehe wote) na mwenzako ni vivyo hivyo. ~Ukiomba huku humemshikilia mtu ndani ya moyo,basi ni heri usingeliomba hata mwenzako naye ni vivyo hivyo ni lazima awe safi. Muombe toba kabla ya kuanza maombi yenu.

(c) Hakikisha mnaelewana vizuri katika semi zenu. ~Yaani isiwe wewe unasema hivi,yeye anasema vile au mara mwenzako anakupinga anataka ya kwake tu ndio yasikilizwe na kufanyiwa kazi. Au isiwe anayakubali ya kwako kishingo upande,yaani ~afanyeje aah basi tu! 

(d) Wote wawili mkubali kuongozwa na Roho mtakatifu. Mjishushe wote wawili na kumruhusu Roho mtakatifu atawale.Epuka story nyingi,zitazuia uwepo wa Bwana.

(e) Ni vyema muwe mnafunga kwa maombi. Kwa maana ikiwa mtaaitabisha miili yenu kwa kuinyima chakula basi ni dhahili mtaweza kuwa pamoja kwa umoja.N.K

ITAENDELEA…

Kwa maombezi,piga sasa +255 655 11 11 49.

Mchungaji G.Madumla.

Beroya bible fellowship church.(Kimara,Dar,TZ)

UBARIKIWE.