Wataalamu wa afya wanashauri ni muhimu binadamu kujua kundi lake la damu ili iweze kumsaidia wakati atakapohitaji kupata matibabu ambayo yanahitaji damu ikiwemo kuwekewa pandikizi za sehemu za mwili. NI vema kujua kundi lako la damu sawa na ilivyo vema kujua mambo mengine yanayochangia kuwa na afya njema.
Aidha, hali hii inatajwa na wataalamu wa afya kuwa inaweza kukuza uwezo wako wa binadamu kufahamu hatari zinazo mkabili kutokana na kundi la damu alilo nalo na kuepuka hatari hizo kwa kutumia mtindo wa maisha unaofaa sambamba na matibabu yanayoweza kutolewa hospitalini.
Hata hivyo, Kama vilivyo viungo vingine vya mwili, damu nayo imetajwa na wataalamu wa masuala ya afya kwamba ina changamoto ya kukumbana na maradhi mbalimbali, magonjwa yanayoathiri utendaji kazi wa damu yanaweza kugawanywa katika makundi kama vile ya kurithi, kuambukiza, mabadiliko ya kimwili na saratani tofauti.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Maabara katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dk. Alex Magesa, ameeleza kuwa damu ya binadamu imegawanyika katika makundi makuu manne ambayo ni A, B, AB, na O, lakini pia makundi haya kutokana na aina ya mfumo kinga wa Rhesus (Rh).
Mfumo huo wa RH umegawanyika zaidi katika makundi madogo kama vile kundi A (hasi), kundi A (chanya), kundi B (hasi), kundi B (chanya), kundi AB (hasi), kundi AB (chanya), kundi O (chanya) na kundi O (hasi) ambapo ameeleza kuwa binadamu yeyote lazima awe na moja wapo ya makundi hayo.
Hata hivyo, amesema kuna aina za protini zinazotakiwa kupewa umuhimu katika uchangiaji wa damu, ikiwemo protini zinazoitwa ABO (blood group) ambapo zipo kabonhaidreti zinazotengeneza kundi la damu A, B, na pia kuna zinazotengeneza makundi mawili (A na B).
Protini ambazo hazina protini A wala B huitwa kundi 0 (Huyu hana protini inayotengeneza A wala B) kwa kiwango kikubwa sana zinachangia kutambua seli mbalimbali za mwili na kwamba mwenye kundi hilo hawezi kumchangia kila mtu.
“Damu inauwezo wa kutengeneza kitu kinachoitwa Ant Bodies, zenye nguvu zaidi kwamaana kama daktari atachanganya kwa bahati mbaya kwenye kuangalia kundi la mgonjwa inaweza kumuua mgonjwa anayeongezewa damu au kumsababishia madhara makubwa" alieleza Dk. Magesa.
Kundi ABO, linatambua protini za kundi la damu A, B, AB au kundi O pia zinaweza kutengeneza kinga “Anti bodies’ ukikosea sasa ndio inaweza kuleta madhara kama damu uliyompa mgonjwa hazioani kuna uwezekano wa kufa moja kwa moja au kumletea madhara kamanilivyosema hapo awali” alieleza Dk. Magesa.
Aidha, ameeleza kuwa makundi yote yenye umuhimu ni yale ambayo daktari akimuwekea mtu/mgonjwa mwingine kwenye upande wa damu huleta madhara kwa kiwango kikubwa ingawa kuna makundi mengi sana, zaidi ya 400 ambayo hayaleti madhara (Makundi hayo hayapimwi kulingana na gharama).
Mbali na hayo ameeleza kuwa katika madhara hayo yanayoweza kupatikana yapo makundi 13 ambayo yana uhuhimu kiasi kwamba mgonjwa ukikosewa kupata huduma anayostahili, anaweza kusababishiwa madhara katika mwili wake.
Makundi ya damu yanayotumika kuwekewa pandikizi za sehemu za mwili
Amesema kuna makundi ya aina mbili yanayotumika sana katika kumhudumia mgonjwa anayehitaji kuongezewa damu na kwamba kundi la kwanza ni ABO na kundi la pili linaitwa Rhesus (RH).
Na pia zipo protini za aina tano kati ya makundi yanayopatikana kwenye kundi la RH ambazo ni C,c, D, E e, inaleta madhara lakini ni madogo lakini kundi D linaweza kusababisha madhara na uwepo wa D chanya (Positive) na kwamba D ni aidha unayo au huna na hivyo ukiandikiwa d (ndogo) ni hasi (Negative). Mfumo wa ABO ambayo kuna aidha ABO, RH ndiyo wanayoangalia zaidi wakati wa kumuwekea mtu damu.
Kwa mujibu wa Dk. Magesa, asilimia kubwa ya wanadamu kwa asilimia 80% wanakundi la D Positive (chanya) na asilimia 15% hawana D Negative (hasi) au RH negative. Asilimia 50% ya wachangia damu katika Hospitali hiyo ya Muhimbili ni kundi 0 na asilimia (20-25) ni kundi A au B na asilimia 5% haitabiriki.
Binadamu ambao hawana RH
Ameeleza kwamba makundi muhimu ya kutolea damu ni ABO/ABH na RH na kwamba kuna mengine muhimu lakini hayana umuhimu mkubwa kama ilivyo hayo mengine ambayo ni H, Lewis (Le), li, P, MNSs, Kell (K), Duffy (Fy), Kidd (JK), Lutheran (Lu).
Kwanini tuna makundi ya damu na yanapatikana vipi?
Dk. Magese, amesema “Haya makundi yote ya ABO na RH ni ya kurithi na hivyo katika maisha yako yote utakuwa nayo kwani huwezi kuyabadilisha na mara nyingi mgonjwa anapewa damu ambayo sio kundi lake na badala yake anapewa ile ya kundi lake linaloshabiana lakini damu haibadiliki na zile seli zilizoingia mwilini mwake baada ya muda zinaondoka baada ya siku 120 na mgonjwa atabakia na damu yake halisi”.
“Umuhimu wa kujua makundi ni pamoja na kujua kuwa upo kundi gani, na wakati wa matibabu ambayo yanahiaji damu ikiwemo kuwekewa pandikizi za sehemu za mwili, kundi la damu litahitajika. “Mfano mtu ana kundi A alafu akapewa kundi B, anauwezekano mkubwa sana wa kufa kwasababu hata figo zitakuwa hazifanyi kazi, atasikia mwili umechemka, wengine wana vimba mwili lakini hii inategemea na jinsi damu zitakavyokukataa” aliongeza Dk. Magesa.
Historia inaonyesha kuwa makundi haya ya damu yaligundulika kutokana na jitihada za wataalamu wa tiba za kujaribu kuokoa maisha ya wagonjwa waliokuwa wanapungukiwa damu katika maneo mbalimbali duniani.
Daktari Mkuu katika Idara ya Magonjwa ya Moyo Muhimbili, Professa Mohamed Janabi, amekaririwa na FikraPevu akisema damu ina mapambano makali dhidi ya magonjwa mbalimbali lakini pia yenyewe huathiriwa kupitia chembe hai, sahani, kwenye uloto ndani ya mifupa nyekundu na nyeupe.
Hata hivyo, ameeleza kuwa “kila kundi lina faida na hasara zake pale tunapoyahusisha makundi ya damu na uwezekano wa kuchangia kutokea kwa magonjwa au kutukinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza na magonjwa ya kuambukiza” alieleza Professa Janabi.
Amebainisha kwamba kwa kipindi kirefu sasa, wanasayansi wa maswala ya afya na tiba wamekuwa wakifanya tafiti mbalimbali kuhusiana na uwezekano wa makundi mbalimbali ya damu kuchochea au kuzuia utokeaji wa magonjwa kadhaa ambayo binadamu anaweza kuyapata.
Aidha, ushahidi wa tafiti nyingi umeonyesha kuwepo kwa mahusiano ya karibu baina ya makundi ya damu na hali ya afya ya mtu.Wataalamu wa afya waliojaribu kuwaongezea watu damu za wanyama au za binadamu wengine, mara nyingi wamekuwa wakipokea matokeo tofauti kulingana na damu anayopewa mgonjwa.
Mwanataaluma wa magonjwa ya binadamu, Shita Samwel, amekaririwa na FikraPevu akisema makundi ya damu yanatokana na urithi wa vinasaba vinavyotofautiana kutoka kwa wazazi wetu.
Alieleza kuwa vinasaba vya urithi vinaweza kuamua kuwepo kwa tofauti za makundi ya damu kwa kutengeneza mifumo tata na iliyo tofauti ya kinga dhidi ya magonjwa katika ukuta wa nje wa chembechembe nyekundu za damu.
Katika utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2006 nchini Thailand, ilibainika kuwa watu wenye kundi la damu la AB, wako katika hatari kubwa ya kupata homa ya Dengue kuliko watu wengine.
Utafiti pia ulibaini kuwa watu wenye kundi A la damu wako katika hatari kubwa ya kupata saratani ya kinywa, tezi za mate na umio. Lakini pia utafiti huo ulibainisha kuwa watu wenye kundi B wana hatari kubwa ya kupata saratani ya koo.
Kundi A pia limekuwa likihusishwa na ongezeko la kutokea kwa saratani mbalimbali ikiwa ni pamoja na ya mishipa ya fahamu, utumbo, mifuko ya mayai, mfuko wa kizazi na mlango wa kizazi kwa wanawake. Tafiti zingine zinabainisha kuwa watu wenye kundi A na B, wana uwezo mkubwa wa kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu, lakini pia watu wenye kundi AB wana uwezo mkubwa zaidi wa kukabiliana na ugonjwa huo.
Tafiti zinaonyesha kuwa watu wenye kundi O la damu wenye vinasaba ya kijenetiki aina ya Adamts7 hawana hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa shambulio la ghafla la moyo kama ilivyo kwa watu wenye makundi mengine ya damu.
Hata hivyo baadhi ya watafiti wanaonyesha kuwa watu wenye kundi la O hawana kinga ya kutosha dhidi ya kipindupindu lakini wana kiasi fulani cha kinga dhidi ya Kifua Kikuu (TB), Malaria isiyo kali, saratani za kongosho, tumbo, matiti na mlango wa kizazi.
Mkazi mmoja wa Dar es Salaam, aliyejitmbulisha kwa jina la Rojas Yeremiah, alipoulizwa kama anajua kundi la damu linalohatarisha afya ya binadamu alisema aliwahi kusikia kutoka kwa ndugu yake kuwa watu wenye kundi la damu la A wanakabiliwa na uwezekano mkubwa wa kupata ugonjwa wa kiharusi.
Licha ya kuwa takwimu zinaonyesha kwamba asilimia kubwa ya Watanzania hawajitokezi kuchangia damu bali wanachangia pale inapohitajika kwa ndugu zao au marafiki, magonjwa mengi yanaweza kuepukwa kwa kuzingatia usafi wa mwili na mazingira, mlo kamili, kufanya mazoezi, kupunguza uzito na kuepuka matumizi ya tumbaku, pombe pamoja na dawa za kulevya.
Uwezo wa kuzaa na kuepuka saratani mbalimbali pia unaweka kuwa nzuri kama magonjwa yasambazwayo kwa njia ya kujamiiana kusiko salama na utoaji wa mimba kiholela, vitaepukwa. Katika tafiti za karibuni wanasayansi wamebaini kuwa kundi lako la damu linaweza kukufanya uwe dhaifu au imara katika kukabiliana na magonjwa fulani.
By Richard Edward å