Tatizo hili husababisha mwanaume kushindwa kumpa mwanamke mimba ambapo hutoa mbegu zisizo na sifa kurutubisha mayai ya mwanamke au kushindwa kabisa kutoa mbegu hizo.
CHANZO CHA TATIZO
Hali ya mwanaume kushindwa kusababisha ujauzito kitaalamu tunaita ‘Failure to Impregnate’ ambayo husababishwa na mambo mbalimbali yanayoathiri utendaji kazi wa mfumo wa mwili na uzazi.
Athari hizo husababisha mwanaume atoe mbegu za kiume zisizo na sifa. Matatizo ya kutokutoa mbegu yanatokana na athari katika kiwanda cha uzalishaji mbegu au korodani. Mbegu zinaweza zisitoke kutokana na njia yake kuziba au zisifike ukeni, yaani zisitoke au zitoke kwa kiasi kidogo sana.
Kiwanda cha uzalishaji mbegu kushindwa kufanya kazi vizuri husababishwa na kuumia korodani, maambukizi sugu mfano magonjwa ya zinaa, kifua kikuu na joto kali. Kusinyaa kwa korodani yaani kuwa ndogo sana, kupotea kwa korodani ambapo mwanaume hana kabisa korodani na magonjwa mengine yanayoathiri mfumo wa homoni mwilini. Magonjwa sugu kama kisukari, kansa na HIV pia huchangia hali hii. Lishe mbovu kwa kutokula vizuri kutokana na kukosa chakula, matumizi ya madawa ya kulevya na ulevi wa pombe ambapo mtu hupoteza hamu ya kula pia huchangia.
Mionzi ya mara kwa mara mfano X-Ray au mionzi ya viwandani, matumizi makubwa ya dawa za homoni kwa lengo la kuongeza nguvu bila utaratibu maalumu pia huweza kuchangia.
Chanzo cha pili ni kuziba kwa njia za kupitisha mbegu ambapo husababishwa na maambukizi, upasuaji katika maeneo ya korodani au henia na kujikuta unaharibu njia za kupitisha mbegu, kuumia korodani, matatizo ya njia ya mkojo na tezi dume.
Chanzo cha tatu ni kushindwa kufanya tendo la ndoa kutokana na kutokuwa na nguvu za kutosha au kukosa kabisa nguvu za kiume. Hali hii huwa na vyanzo mbalimbali kama tulivyozungumzia katika matoleo yaliyopita.
Lakini kasoro za uume na kuwahi kumaliza tendo la ndoa pia huchangia.
DALILI ZA TATIZO
Mwanaume mwenye tatizo la uzazi huwa na dalili mbalimbali, mojawapo ya dalili hizo ambazo moja kwa moja ni viashiria vya kuwa na tatizo ni kama vile kutotoa kabisa manii wakati wa tendo.
Pia maumivu ya njia ya mkojo na mkojo kutotoka vizuri mara kwa mara, kasoro za kimaumbile katika uume au korodani, kuondolewa tezi dume, kutoa manii lakini zikakosa mbegu, kutoa mbegu chache zisizokidhi kiwango.
Matatizo ya mbegu huwa yanagunduliwa hospitali baada ya uchunguzi wa kina. Kuhusu maambukizi ya mara kwa mara ya njia ya mkojo kwa mwanaume inashauriwa pia na mwenzi wako atibiwe, vinginevyo naye atapatwa na maambukizi ya mara kwa mara ukeni.
UCHUNGUZI
Mwanaume mwenye tatizo la uzazi ana historia ya kukaa na mwanamke kwa angalau mwaka mmoja wanatafuta mtoto lakini hawapati. Mwanaume ataanza kuonyesha dalili kama tulizozieleza au asiwe nazo. Tatizo hili la uzazi kwa mwanaume halijalishi kama tayari una watoto au huna tatizo katika ufanyaji wa tendo la ndoa.
Vipimo mbalimbali vitafanyika kwa daktari bingwa wa matatizo ya uzazi katika hospitali kubwa za mikoa.
MATIBABU
Baada ya uchunguzi wa kina ambapo mwanaume atapimwa mkojo, vipimo vya damu huangalia vichocheo na maambukizi, pia mhusika atapimwa manii kuangalia matatizo mbalimbali pamoja na sifa za mbegu za kiume kama zipo. Vipimo na tiba itategemea matokeo na jinsi daktari atakavyopanga.