25.06.2017: MH. BISHOP DR. GERTRUDE RWAKATARE ALIVYOKEMEA MAPEPO NA MAJINI SIKU YA JUMAPILI KATIKA IBADA YA KUONDOA NJAA - MLIMA WA MOTO MIKOCHENI "B"
Wapendwa katika BWNA, kuna ndugu zetu huko mitaani wanateseka, wamefungwa na nguvu za giza, wametawaliwa na roho chafu, kila jambo wanalofanya halileti mafanikio, wengine wana mali nyingi lakini bado wanateseka kwa magonjwa na shida mbalimbali. Watu wametawaliwa na changamoto mbalimbali hawaoni mlango wa kutokea, kila wakijitahidi kufanya kazi kwa bidii hawaoni matunda yake.
Watu hawa wanaopitia changamoto za kimasha tunaishi nao mitaani mwetu na majumbani mwetu, wanatamani kuwa na maisha ya amani na furaha lakini wanakosa mtu wa kuwaongoza katika nuru. Wengine wanatamani kuokoka lakini kila wakijitahidi kuchukua maamuzi shetani anaingia na kuondoa ile hamu ya kuokoka, wengine wanajiita wameokoka lakini unashangaa bado wanashambuliwa na mapepo na magonjwa mbalimbali.
Tuna kila sababu ya kurudi kwa Mungu na kumuomba aondoe hii hali ambayo watu wake wanapitia, wanateseka, wanakosa furaha, amani katika maisha yao. Wamekuwa ni watu wa kulia, wengine wamekata tamaa ya maisha wamebaki wakisubulia kifo, wanahangaika na kila wakiangalia mashariki, magharibu kusini na kaskazini hawaoni mtu wa kuwasaidia.
Hakuna mtu anayetamini kuishi maisha kama haya ya mateso, kila mtu anatamani kuishi maisha ya amani na furaha. Watu hawa wanahitaji sana msaada wako wa maombi, wanahitaji Neno la Mungu kupitia kinywa chako, wanahitaji faraja kutoka kwako, wanahitaji uwaongoze njia sahihi ya kumjua Mungu, wanahitaji kuondoka katika giza na kuiona nuru, wanahitaji kuokoka, wanahitaji kushikwa mkono katika mapito wanayopitia.
Mungu amekupa uhai, maarifa, mali, elimu, kipaji, karama, maisha bora, upako katika kazi ya Mungu, huduma nzuri na baraka nyingi. Baraka ulizopendelewa na Mungu zinahitajika sana kuwasaidia wengine ili nao wabarikiwe kama wewe. Kumbuka na wewe ulipokuwa unapitia haya yote kuna watu waliweza kukuombea, hata kama hukuwaona wakikuombea ila tambua kuna watu walitamka maneno ya uponyaji na ukawa mzima, sasa ni zamu yako kuwaombea hawa ndugu zetu na kuwasaidia.
Angali ni kitu gani ambacho Mungu amekubariki nacho na kitumie kusaidia wengine ambao hawana. Kama umebarikiwa na mali nyingi basi wasaidie wenye uhitaji, kaka wewe ni mtumishi wa Mungu waombee wenye uhitaji wa maombi, kama wewe una karama fulani basi itumie kwa kazi ya Mungu ili kusaidia wengine kuimarisha imani zao kwa Mungu wetu, kama wewe una maisha bora wasaidie maskini nao waishi maisha bora. Kwahiyo kila mtu aangalie ni eneo gani Mungu amembariki na alitumie eneo hilo kuwabariki wengine.
Wewe ni wa thamani kwa kazi ya Mungu, wewe unaweza kubadilisha maisha ya mtu kupitia kinywa chako kwa kuwaombea, wewe ni mtumishi wa Mungu kama watumishi wengine, jitambue na fanya maamuzi sasa ya kumtumikia Mungu kwa kuwasaidia wengine kupitia karama yako.
Siku ya Jumapili 25.06.2017 katika ibada ya KUONDOA NJAA majumbani mwetu iliyofanyika katika kanisa la Mlima wa Moto Mikocheni "B" tumeona Mungu akiondoa mapepo kwa watu kupitia watumishi wake katika kipindi cha MOMBEZI kilichoongozwa na Bishop Dr. Gertrude Rwakatare wakishirikiana na Mch. Noah Lukumay..
Watu wengi sana waliweza kubebwa na kupelekwa madhabahuni kwaajili ya kuombewa. Ilikuwa ni ibada iliyojaa upako na uwepo wa Mungu. Tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kutokana na ule upendeleo alioweka katika nyumba yake ya Mlima wa Moto Mikocheni "B". Watu waliweza kufunguliwa kutoka katika mateso yao mara baada ya mtumishiwa Mungu Mh. Bishop Dr. Gertrude Rwakatare kuwagusa kwa mikono yake na kuwaombea. Mch. Noah Lukumay akishirikiana na watumishi wa Mungu waliweza kuwaombea na kukemea mapepo na nguvu za shetani zilizokuwa zikiwasumbua watu kwa kipindi kirefu. Watu wengi sana walifunguliwa na kuweka huru kwa Jina la Yesu Kristo.
Yawezekana na wewe hapo ulipo unapitia mapito magumu sana na huoni mtu wa kukusaidia, nakuomba Jumapili hii au katikati ya wiki usikose ibada zetu na utaona mkono wa Mungu katika maisha yako. Mungu akubariki sana.