RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

27.08.2017: WATU WALIOAMUA KUOKOKA NA KUBATIZWA KATIKA KANISA LA MLIMA WA MOTO MIKOCHENI "B"

Watu wanazidi kumpokea Yesu Kristo kuwa BWANA na Mwokozi wa maisha yao. Tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa mambo anayoyafanya katika kanisa lake la Mlima wa Moto Mikocheni "B" kupitia mtumishi wake "Mh. Bishop Dr. Gertrude Rwakatare na watumishi wote wa kanisa hili. Tunaona watu wengi kutoka pande mbalimbali za dunia wakifika katika nyumba ya BWANA ya Mlima wa Moto Mikocheni "B" wakihitaji kuokolewa. Na tumekuwa tukishuhudia kwa macho yetu jinsi watu wanavyookoka kila itwapo Jumapili. 


Katika ibada ya Tamasha la Maombezi iliyofanyika siku ya Jumapili 27.08.2017 tulishuhudia watu wengi wakihitaji kushikwa mkono na Mungu ili aweze kuokoa maisha yao.

Watu wengi waliokoka siku ya Jumapili na kuongozwa sala ya toba na Mch. Francis Machichi na baada ya kuongozwa sala ya toba, Mch. Noah Lukumay na jopo la wachungaji waliweza kuwaombea waongofu wapya. Wakati wanaombewa baadhi yao walitokwa na nguvu za giza na kupiga kelele huku wakilia wakihitaji msaada kutoka kwa Mungu. Mapepo na majini yalikuwa yakiunguzwa na moto wa Mungu ulao.

Baada ya kuombewa Mh. Bishop Dr. Gertrude Rwakatare aliweza kuwapa Neno litakalowasaidia katika safari yao ya wokovu na aliweza kuwaombea. Pia aliwagawia fomu za kujiunga na kanisa la Mlima wa Moto Mikocheni "B".

baada ya ibada kumalizika, waliweza kubatizwa kwa maji mengi kama vile Yesu alivyobatizwa na Yohana. Wakati wakibatizwa baadhi yao walianza kulipuliwa mapepo na majini huku wakipiga kelele wakihitaji nguvu za Mungu ziwaokoe katika mateso wanayopitia. Roho Mtakatifu aliwashukia na kuingia ndani yao ili awe msaada na kiongozi wa maisha yao mapya ya wokovu

Siku ya Jumatatu walianza masomo ya kukulia wokovu katika kanisa la Mlima wa Moto Mikocheni "B". Masomo yalianza saa 9 alasiri.

Watu hawa wanahitaji sana maombi yako, kwani kwa sasa wameanza safari ndefu na katika safari hii kuna maadui wengi sana wanaotaka waanguke katika wokovu ili wasisonge mbele. Maombi yako yatawafanya kuwa imara KIIMANI mpaka pale watakapoweza kujisimamia wenye katika wokovu.

Yawezekana na wewe unatamani kuokoka na kubatizwa kwa maji mengi, tunakukaribisha katika ibada ya Jumapili hii Mlima wa Moto Mikocheni "B" saa 3 asubuhi hadi saa 8 mchana. Na siku za katikati ibada inaanza saa 9 alasiri hadi saa 1 jioni.

Siku ya Jumapili usafiri ni bure kuanzia kituo cha mabasi cha Makumbusho au Mwenge kwenye mataa, utaona magari yetu. Baada ya ibada utarudishwa kituoni.




















































Comments