Mh. Bishop Dr. Gertrude Rwakatare siku ya Jumapili 17.09.2017 katika kanisa la Mlima wa Moto Mikocheni “B” kwenye ibada ya KUFUFUA VITU VYETU VILIVYOKUFA (Habakuki 3:2) alikuwa na haya ya kusema, “Yule Yesu mtenda miujiza yupo katikati yetu. Kila mateso, kila huzuni, kila shida vikutoke kwa jina la Yesu Kristo. Leo ni siku yako ya muujiza, Baraka na kuguswa na BWANA. Ukipata muda somo Nahumu 1:9 inasema, “Unawaza nini juu ya BWANA?” Jiulize hapo ulipo, “Unawaza nini juu ya BWANA?” Pengine unapitia changamoto Fulani au tatizo Fulani lakini lazima ujiulize, “Unawaza nini juu ya BWANA?” Pengine unafikiria BWANA amekusahau, amekuacha, au unafikiri unapoteza muda wako unaotumia kumwabudu Mungu wako kanisani. BWANA anasema, “Atakomesha kila mateso, misukosuko, kwahiyo usihofu kwani atakomesha kila dhoruba na utakuwa huru kwa jina la YESU, Mungu atakupa kulingana na haja ya moyo wako.
Endelea kumtumikia Mungu kila kuitwapo leo, naye atafungua milango ya mafanikio katika kazi yako, ajira yako, mahusiano yako, ndoa yako, afya yako, familia yako. Atakukinga na wabaya wako, wachawi, mapepo, majini. Ataondoa ndoto mbaya, roho chafu, vitu vinavyosababisha usisonge mbele na mengine kama hayo.
Kuvishindi vita dhidi ya maadui zetu inatokana na wewe kusimama imara kwa BWANA kwa kuyafanya yale anayokuagiza, kufanya maombi, kutumikia kwa moyo wako wote, kuwatii watumishi wa Mungu, kusoma Neno la Mungu, kuitangaza Injil, kuwapenda watu wote, kuwasaidia wenye uhitaji, kutowakwaza wengine kwa maneno mabaya, kushika amri kumi za Mungu na kuzifanyia kazi.
Mungu anakupenda, anatamani kukuona unaishi maisha ya furaha. Anasikitika sana anapoona unataabika na hutaki kumrudia. Utakapoamua kumrudia naye atayabeba matatizo yako na utakuwa huru. Amini kila kitu unachoambiwa na watumishi wa Mungu au kile unachokisoma katika Biblia na kifanyie kazi.
Wewe ambaye hukufika katika ibada ya Jumapili, tunakualika katika ibada ya Jumapili ijayo itakayoanza saa 3 asubuhi hadi saa 9 mchana. Usafiri ni bure kuanzia kituo cha mabasi cha Makumbusho au Mwenge kwenye mataa barabara ya Coca Cola. Baada ya ibada utarudishwa kituoni.
Mh. Bishop Dr. Gertrude Rwakatare
Comments