RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

Redio yafungiwa baada ya mchungaji kusema ‘wanawake chanzo cha matatizo duniani’

Serikali ya Rwanda kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Mawasiliano nchini humo (RURA), imekifungia kituo cha redio ya kidini cha Amazing Grace 105.1 FM kurusha matangazo kwa kipindi cha mwezi mmoja pamoja na kulipa faini ya faranga milioni 2 sawa na Tsh milioni 6, baada ya redio hiyo kurusha matangazo yaliyowadhihaki wanawake kwa kuwataja kuwa ndiyo chanzo cha matatizo duniani.


Mamlaka hiyo imeeleza kuwa mnamo Tarehe 29 Januari 2018 Mchungaji wa Kanisa la Kisabato, Niyibikora Nicholas akitangaza injili kupitia kituo hicho cha redio alisikika hewani akisema wanawake ni moto wa kuotea mbali kwani ndo chanzo cha maovu na migogoro isiyoisha duniani.


Mchungaji huyo akiwa LIVE hewani aliendelea kusema kuwa hata Mungu hawapendi wanawake, kwani mwanamke hajawahi kuwa mtu mwema tangu enzi za bustani ya edeni ambapo alikula tunda alilokuwa ameambiwa asile na kumshawishi na mumewe kufanya dhambi.

Mamlaka hiyo ilichambua mahubiri yake yote ambapo imeeleza kuwa maudhui yote yalitoa mifano lukuki ya kwenye biblia inayowaelezea wanawake kuwa ni watu wabaya huku mchungaji huyo akiwataka wanaume wasiwaamini wanawake kwani wanawake ni watu wabaya.

Mhubiri huyo alizua mjadala mzito kwenye mitandao ya kijamii nchini Rwanda na kuwakasirisha wanawake ambapo Mwavuli wa Utetezi wa Haki za Wanawake Rwanda (Profemmes Twese Hamwe) na Jukwaa la Waandishi wa Habari wa Kike Rwanda (ARFEM) walipaza sauti zao kutaka achukuliwe hatua kwa tuhuma za uchochezi wenye misingi ya kijinsia na kulenga kusababisha mtafaruku kwenye jamii.

Tayari Ofisi ya Mwendeshaji Mkuu wa Mashtaka imeliagiza jeshi la polisi kitengo cha upelelezi wa makosa ya jinai kuanza upelelezi juu ya madai yanayomkabili Mchungaji huyo.

Comments