BAADA ya tetesi kuzagaa kila kona kwamba staa wa muziki wa Injili Bongo, Joel Lwaga anaishi kinyumba na msanii wa filamu nchini ambaye pia anaimba muziki wa Injili, Rose Alphonce ‘Muna’, viongozi wa muziki huo wameibuka na kueleza mazito, Risasi Mchanganyiko linakupa mkanda kamili.
Awali, baada ya hivi karibuni mtoto wa Muna kufariki na kutokea kwa migogoro mingi kati ya mwanamama huyo na mumewe Peter Zacharia, habari nyingine iliyotawala kwenye mitandao ya kijamii ni ya Muna kudaiwa kuwa alikuwa akiishi kinyumba na mwimba injili huyo.
Wapo ambao wanadai hata mpaka sasa wawili hao wanaendelea na urafiki wao kwani wote wako nchini Kenya wanakofanya huduma huku Muna akiwa hajafikisha hata siku arobaini tangu mwanaye afariki dunia.
“Yaani huyu Muna anaonekana bado anaendelea na uhusiano wake na Joel maana hivi juzi tu amemfuata huko Kenya ambako anafanya huduma ya uimbaji huku akisingizia kuwa ana ziara ya makanisani kutoa ushuhuda,” kilisema chanzo ambacho kiko karibu na Muna.
Ili kuujua ukweli na utaratibu ukoje kwa watumishi wa Mungu kama hao wanapotajwa kuishi pamoja kabla ya ndoa, Risasi Mchanganyiko lilimtafuta Rais wa Tanzania Music Foundation, Dk. Donald Kisanga wanaoshughulika na usimamizi wa waimbaji wa muziki wa injili ambaye alisema kwamba wao wamekuwa wakisikia tu tetesi hizo lakini ukweli wake hawajaupata.
“Tumekuwa tukisikia tu kwamba Joel na Muna wanaishi kinyumba lakini bado hatujapata ukweli wa hili jambo maana ni muda mrefu tunawaona wako kwenye kila huduma pamoja nasi tunawachukulia ni marafiki tu.
KUFUNGIWA MUZIKI
“Sasa baada ya tetesi hizo kuzidi, kamati yetu ya maadili ipo kazini kwa sasa kufanya uchunguzi kama kweli wanaishi au walikuwa wanaishi pamoja au laa na endapo itathibitika kuwa ni kweli tutawafuta uanachama pia kuwafungia kuimba maana wanachafua waimbaji wote wa injili ambao wanaaminika ni watumishi wa Mungu.
“Tunamshauri huyo Joel kuwa makini kama huyo Muna kweli ni mke wa mtu na hajapewa talaka aachane naye hata kama ni mchumba wake kama inavyosemekana kwani akiendelea kung’ang’ania itamletea matatizo,” alisema Dk. Donald.
Muna hivi karibuni alifiwa na mtoto wake, Patrick Peter ambaye alikuwa akipatiwa matibabu nchini Kenya ikiwa ni baada ya kugundulika kuwa alikuwa na uvimbe kwenye Ubongo, ambapo wakati wa matibabu walikuwa nchini humo pamoja japokuwa mwanamama huyo alidai kwamba alimkuta huko kwani alikuwa kwenye shughuli zake za uimbaji.
STORI: Gladness Mallya, Risasi Mchanganyiko
Comments