RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

KANISA KATOLIKI KUANZA MCHAKATO WA KUMTANGAZA SOKOINE MWENYE HERI

Kardinal Pengo,kiongozi wa kanisa katoliki Tanzania.


Marehemu Edward Moringe Sokoine enzi za uhai wake.
Askofu wa Jimbo Katoliki Mororogo, Telesphor Mkude amesema uadilifu na ucha Mungu wa aliyekuwa Waziri Mkuu, marehemu Edward Sokoine unatosha kuanza mchakato wa kumtangaza kuwa mwenye heri.
Akitoa mahubiri katika kumbukumbu ya miaka 28 ya kifo cha Sokoine, yaliyofanyika jana katika eneo alilopata ajali la Wami Dakawa Sokoine, Askofu Mkude alisema marehemu aliwajali wanyonge hali ambayo aliona ingetosha kumuwezesha kuanzisha mchakato huo ndani ya kanisa hilo katoliki ambalo alikuwa muumini wake
Mkude alisema wema wa Sokoine ulionekana kwa macho ya wanadamu na kwamba, Mungu pia kwa kutumia vipimo vyake alimwona ndiyo maana ndugu, jamaa, marafiki na waumini wenzake wameona kuwa iko haja ya kumwombea kiongozi huyo.

“Ingawa mwenzetu amekwisha tangulia mbele za haki lakini, kwetu sisi leo hii tumekutana hapa ili kumwomba Mungu kupitia sadaka ya misa takatifu ili kuweza kumtakasa marehemu ili kama kuna dhambi zozote basi Mungu aweze ‘kuzifuta," alisema Askofu Mkude.

Kwa upande wake Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliunga mkono hoja hiyo ya Askofu Mkude na kumtaja hayati Sokoine kwamba, alikuwa ni kiongozi wa mfano kutokana na misimamo yake kipindi alipokuwa waziri mkuu.

Waziri mkuu Pinda alisema misimamo hiyo ya Sokoine ilikuwa ikimtia moyo Baba wa Taifa hayati, Mwalimu Julius Nyerere kwa kuona kuwa alikuwa na kiongozi aliyetenda kazi kama alivyotaka.

Alisema yeye (Pinda) alipata bahati ya kufanya kazi na hayati Sokoine hivyo, alipata fursa nzuri ya kuona mambo aliyokuwa akiyafanya kiongozi huyo hali iliyomfanya kuona kuwa misimamo yake katika kazi ilifanana na ile ya Mwalimu.

“Alichokisema baba Askofu hata mimi nilikuwa nikikiwazawaza, kutokana na ukweli kuwa Sokoine alikuwa ni mchapakazi lakini pia mchamungu. Japo kuwa sisi wakatoliki mpaka kufikia kutangazwa mwenye heri inaweza kuchukua hata miaka 100 lakini wenzetu husema ‘Inshallah’ siku moja atatangazwa kuwa na sifa hiyo,” alisema Pinda.

“Sokoine alikuwa akifanana sana na Mwalimu, si tu katika masuala ya dini lakini pia katika misimamo yake katika kuchukia rushwa, kuchukizwa na walanguzi na kuwapenda watu wa kipato cha chini,” alisema Pinda.

Alisema Sokoine alikuwa ndiyo kiongozi wa kwanza aliyeanza kusimamia mageuzi ya kilimo kutoka katika jembe la mkono na kwenda katika matumizi ya trekta, hatua hiyo ilikuwa kwa kutambua kuwa Watanzania karibu asilimia 80 ni wakulima.

Kwa upande wake mtoto wa marehemu ambaye pia ni Mbunge wa viti Maalum, Namelok Sokoine, licha ya kuwashukuru viongozi, jamaa na marafiki walioshiriki katika kumbukumbu hiyo ambayo hufanyika kila mwaka ifikapo April 12, alisema baba yao mzazi licha ya kutokuwa naye lakini aliwaachia kumbukumbu ya sala ambayo ilitumwa katika familia yao mwaka 1985 na shirika la Francis De Sales ambalo Sokine alijiunga nalo.

Watu wengine walioshiriki katika kumbukumbu hiyo iliyotanguliwa na riadha iliyowajumuisha wananchi mbalimbali walikuwa ni pamoja na waziri mkuu aliyejiuzulu Edward Lowassa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri ya Mkuu (Uwezeshaji na Uwekezaji) Dk Mary Nagu, Waziriwa Nchi, Ofisi ya ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia na mwenyekiti wa Chamdema Freeman Mbowe.

source--gazeti mwananchi.

Comments