RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

MFUMUKO WA VYAMA VINGI NI SABABU YA KUPOROMOKA KWA UCHUMI WA NCHI:MCHUNGAJI KALATA

Wananchi wakiwa katika moja ya mkutano wa kisiasa

NA MWANDISHI WETU

MFUMUKO wa vyama vingi vya siasa umebainika kuwa ni sababu kubwa iliyosababisha kuporomoka kwa uchumi wa nchi. Mwito huo umetolewa na Mchungaji Christosiler Kalata wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri(KKKT),Usharika wa Matumbi jijini Dar es Salaam leo.

Alisema kuwa vyama hivyo vimekuwa vikitumika kama chachu ya kukwamisha kasi ya maendeleo ya nchi hasa kwa kujiendesha kibinafsi,ikiwa ni pamoja na kukata tamaa, jambo linaloashiria ufinyu wa maendeleo ya wananchi.

Vile vile alihoji kuwa ikiwa serikali iliziruhusu taasisi mbalimbali kuanzisha vyuo,kwa ajili ya kuendeleza vipaji vya vijana kwa lengo la kupata wataalamu, badala yake elimu hiyo wanaitumia kwa kushikilia madaraka kibinafsi.

“Hatari ninayoiona, ubinafsi umetawala, uchoyo, uvivu, tamaa ya kutajirika haraka, kazi za mikono ziko wapi? Leo Maprofesa wamekata tamaa, siasa sasa hivi imekuwa rungu la mwisho la kuiua nchi”.

Alieleza kuwa endapo wataalamu hao wangetumia vema elimu wanayoipata ingeweza kusaidia katika sekta mbalimbali hususan katika kubuni bidhaa zenye nembo ya Tanzania.

“Kinachotokea sasa Tanzania ni nini? Hakuna ubunifu bali tunashuhudia maneno yasiyo na vitendo, na wengine wameona siasa ndiyo ajira yao, na kuamua kuingia huku, tena wakitukanana baina yao na wengine kwa kuneneana maneno mabaya huku kila mmoja akipigania ajira yake.

Aidha, alichanganua kuwa licha ya serikali kuingia katika mikataba mbalimbali na nchi za nje lakini mikataba hiyo imekuwa ni sababu ya kubadilisha mifumo ya nchi na kuingia katika mifumo yao hasa wa vyama vingi vya siasa.

Mchungaji Kalata anafafanua kwamba mmongo’onyoko huo umesababisha maafa katika demokrasia, hasa kwa kukosa muongozo wa kulinda rasilimali za nchi.

Source: fullshangweblog.com

Comments