RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

MAISHA HAYA SITAYASAHAU KAMWE

Muacheni Mungu aitwe Mungu, nayakumbuka maisha haya, natamani kulia. Nimeteseka sana!!! Kushinda bila kula kwangu ilikuwa na kawaida, nikipata mihogo asubuhi kwangu ni muujiza. Nilitaabika sana. Maisha haya yatabu yalianza nilipomaliza kidato cha sita. Ndipo nilipoamua kuishi maisha ya gheto. Nilimuomba rafiki yangu Japhate anisaidie mahali pa kulala, alinikubalia na nikaishi naye kwa kipindi cha miezi kama mitatu. Niliugua sana mpaka ikafika wakati nikatamani kufa kutokana na taabu nilizokuwa nazipata. Kumbuka rafiki yangu alikuwa anaishi maisha ya gheto na hamtegemei mtu yeyote kupata chakula, akikosa na mimi nimekosa. Ila mwenzangu alibahatika kwani nyumba aliyekuwa anaishi ilikuwa ni nyumba ya baba yake, ambaye alihamia Mbeya, na hivyo kumuachia  mwanae na kaka yake.

Nikiwa katika maisha ya gheto na rafiki yangu Japhate pale Kurasini, niliugua sana malaria na nikakonda sana, na hii ilisababishwa na kukosa chakula an ugonjwa uliokuwa ukinisumbua, nilisongwa na mawazo kiasi kwamba nilitamani kurudi kijijini kwangu lakini nikawa sina hata nauli na sikupenda kurudi kijijini. Mawazo yakawa ni mengi sana kuhusu mapito niliyokuwa napitia.

Kulia ni rafiki yangu Japhate aliyenihifadhi nyumbani kwake baada ya kumaliza kidato cha sita. Hapa tulikuwa katika Birthday ya classmate wetu Mwita

Baada ya kuona hali yangu ni mbaya kiafya nikamwomba rafiki yangu mwingine anayeitwa Makoye ambaye nilimaliza naye Jitegemee High School na nilisoma naye Njombe secondary miaka ya 1998 na  anatokea mafinga ambako ni nyumbani kwa kaka yangu ambaye kwa sasa siko naye duniani. Makoye alinikubali na akaamua niishi naye katika gheto lake. Maisha yakawa bado si mazuri kwani wote tulikuwa hatuna kazi na tunategemea kupata chochote kutoka kwa ndugu zetu waishio mikoani. Mara zingine tunaona aibu kuwaomba pesa za matumizi na inatulazimu kutafuta njia zingine za kuishi. Ilifika kipindi misaada ikakata kwani nao walijua kuwa tumekuwa na tuna elimu ya kutosha na tunaweza kujitegemea. Ndugu yangu tulitaabika sana, hasa mimi nilidhoofika sana. Rafiki zangu walidhani labda ni "Ngoma/ UKIMWI kutoka na kukonda, mwili unanuka kikwapa, nilijiona mimi kama nimelaaniwa.
Maisha yakiwa magumu sana, maombi yalikuwa ndio chakula changu. Hapa nilikuwa katika Birthday ya rafiki yangu Mwita maeneo ya Tabata. Niliombwa niaombee chakula.

Kipindi hicho ndicho kipindi ambacho nilikuwa karibu sana na Mungu wangu, lakini nilikuwa sina kanisa la kuabudu. Nilipokuwa nasoma Jitegemee nilikuwa naishi bwenini kwahiyo ibada zetu zilikuwa ni hapo hapo shuleni. Rafiki yangu Makoye akanishauri niwe na kanisa la kuabudu, ndipo aliponialiaka katika kanisa lao la CCC. Imani yangu ilizidi kuongezeka na nikawa na matuamini kuwa sasa maisha yangu yanaenda kubadilika. Nilibarikiwa sana na maombezi na mafundisho ya hapo kanisa.

Siku moja nikakorofishana na rafiki yangu Makoye, tukachukiana sana, na wakati huohuo tunakaa chumba kimoja na tunalala kitanda kimoja. Kukawa hakuna mazungumzo mazuri kati yangu na yeye, kimia kiltawala, mambo yanaenda kwa ishara tu. Kama mimi nikipata fedha kutokana na mihangaiko, nanunua chakula cha kwangu na yeye akipata fedha ananunua chakula chake tu. Maisha hayo yalitusumbua sana hasa kutoelewana kati yetu na tunaishi pamoja. Shetani akaanza kuingia kidogo kidogo akitaka dhambi ya choyo itutawale. Namshukuru Mungu hali ya kuchukiana ikaisha na tukaelewana na kuwa marafiki wazuri sana.

Unapopitia magumu, Mungu anakupa akili ya kutatua hayo matatizo yako. Siku moja nikapiga simu kwa kaka yangu ambaye kwa sasa ni marehemu kwa sasa, Amir sanga-nikamuomba anisaidie kodi ya chumba nipange. Kaka kwasababu alikuwa ananipenda alinisaidia kodi ya mwaka.

Marehemu kaka yangu Amir Sanga akiwa katika duka lake la jumla mkoani Iringa-Mafinga

Nikatafuta chumba cha Tshs 15, 000 maeneo ya Sinza Kijiweni kwa mama Macha. Chumba hicho kilikuwa hakina dari, madirisha ni mabovu, hakijapigwa sementi. Niliamua kuingia na kuanza maisha ya kujitegemea na bila ya kutegemea rafiki au ndugu. Nilimshukuru sana Mungu kwa kupata mahali pa kuishi, niliyafurahia maisha hayo kwani nilikuwa na uhuru zaidi. Maisha yalikuwa magumu sana, sina msaada wowote na mimi sikutaka ndugu zangu kuwa naishi maisha ya taabu. Nilijiamini!!!. Nilikaa muda wa mwaka mmoja sina kazi, nikawa ombaomba. Nikipata 500 kwangu ilionekana kama 10000. Mia tano ilinisaidia kupata mihogo ambayo nakula asubuhi kidogo na jioni.

hapa nikiwa na watoto wa mama mwenye nyumba na majirani, ni kipindi nilichofikiria kwenda kubatizwa, na hii picha ilipigwa na huyo dada ambaye ni jirani yangu, ambaye alipenda nipige naye picha

Siku moja nikiwa nimekaa nje, nikamkumbuka sana Mungu, nikatamani kubatizwa. Ilipofika Jumapili nilienda kanisa la Sinza Christian Centre lililoko Sinza. Mchungaji aliposema watu wanaotaka kuokoka waje mbele, nilienda bilaya kushauriwa na mtu, niliombewa sana na baada ya ibada nilipelekwa bahari ya Hindi kubatizwa. Nilifuahi sana baada ya kubatizwa.
Nikiwa na rafiki yangu Gelasi (kushoto) ambaye alikuwa msaada mkubwa sana. Wakati sina kitu yeye alikuwa mwepesi kunikopesha na kunisaidia fedha. Alikuwa anauza duka na kaka yake. Kwa sasa na yeye ni mjasiliamali, kwani kapitia magumu akiwa na kaka yake.

Maisha yangu yalianza kubadilika baada ya kumpokea Mungu wangu, nikapokea simu kutoka kwa kaka yangu kuwa nitafute shule ya kompyuta wakati nasubiria majibu ya kidato cha sita. Nilitafuta chuo na kukipata Chuo Cha IIT kilichopo Posta Dar es Salaam. Nikasoma hapo na kupata Advance Diploma ni Computer Studies. Baada ya kuamliza masomo ya kompyuta nikaomba kazi ya kufundisha katika chuo cha City Computer Academy. Mshahara wangu ulikuwa 50,000 kwa mwezi. Pesa hiyo ilionekana kubwa sana kwangu, ukifananisha na maisha niliyokuwa naishi huko nyuma. Nilifanya kazi mahali pale na baada ya muda wa mwaka mmoja nikakorofishana na uongozi wa chuo, kwani wakawa wanataka mshahara wangu kupunguzwa, niliumia sana na kuanza mchakato wa kutafuta sehemu nyingine ya kufanya kazi. Sababu kubwa ya mshahara wangu kupunguzwa ilitokana na mimi kuomba kuanza kufundisha Party time, kwani kaka yangu alinambia nijiunge na chuo cha IFM kwaajili ya kuchukua kozi ya Social Protection.
Rulea sanga nikiwa Mwalimu katika Chuo cha CCA. na hiki ndicho chuo cha CCA Posta

Kaka yangu enzi ya uhai wake alikuwa anapenda sana elimu, ndio maana alikuwa ananiandaa ili niwe msomi na niyaendeshe maisha yangu vizuri. Niliuambia uongozi kama mtapunguza mshahara itabidi niache kazi kwani 50,000 hainitoshi kutokana na nauli na chakula kwa mwezi. Niliamua kwenda katika chuo nilichosoma kompyuta cha IIT na kuomba kufundisha, nilikubaliwa na nikawa mwalimu wa Party Time. Nikiwa hapo nafundisha niakawa pia nasoma IFM. Hali ilikuwa ngumu sana, kusoma na kufundisha, lakini nilivumilia kwani nilijua nini nakifanya. Mungu alinipigania nikamaliza masomo yangu na nikafaulu.

Nilipomaliza masomo yangu na kupata degree ya Social Protection, nikaanza kutafuta kazi. Huu ulikuwa ni mguu sana kwangu kupata kazi. Niligonga kila ofisi inayojishughulisha na Hifadhi ya jamii bila ya mafanikio, mpaka leo hii naandika haya, sijawahi kufanyia kazi elimu yangu ya IFM.

Nikiwa nasoma, malengo yangu yalikuwa kuwa mjasiliamali na sio kuajiliwa, lakini nikawa nashindwa nitaanzaje. Nikiwa bado nafundisha, siku moja mzungu alikuja pale shuleni na kuniomba niwe nawafundisha watoto wake nyumbani kwake kama party time, nilimkubalia yule mzungu na nikitoka darasani kufundisha nikawa nawahi Masaki kufundisha. Niliendelea na hali hiyo mpaka nilipomaliza kuwafundisha. Mzungu yule akaniuliza, "Unafurahia kazi unayofanya?" nilimjibu "Hapana" akanambia, "Mimi nina mkwe wangu ameanzisha ofisi yake ya Graphics, ungependa kufanya naye kazi?" Nilimkubabali, baada ya muda akanambia niende nikaongee naye, na nilipofika, Mungu alivyo waajabu. yule mzungu Ulric aliniuliza nipeleke kazi zozote ambazo nimewahi kufanya za graphics. siku iliyofuata nilizipeleka na yeye alizipenda sana na kuniuliza tukulipe shilingi ngapi? Nikawambia yoyote unayofikiria itanisaidia. Ulric alinambia nitakulipa 1,100,000 tukijumlisha kodi zote kama kianzio kwako. Unajua nilishtushwa sana na kutoaamini nilichoambiwa. Kumbuka nilipokuwa CCA nililipwa 50,000, nilipokuwa IIT 450,000 na sasa 1,100,000 kwahiyo mwisho wa mwezi nikawa natoka na 750,000, na hiyo ilikuwa na mshahara wa kuanzia kazi.

Nikiwa na graphic designer mwenzagu, Hanesy katika kampuni ya Roots
Mungu hakuniacha hapo, ndipo ankanipa maono ya kuanzisha tovuti yangu ya RUMATZ ambayo kwa sasa haifanyi kazi. Website hii ilikuwa inajihusisha na habari za Mungu, na ilipendwa sana na watu.

Mungu akaanza kufungua milango ya ujasiliamali na kunipa ujasili na kuniondolea hofu. Siku moja nakumbuka niliamua kuongea na rafiki yangu ambaye kwa sasa ni kiongozi wa Band ya Glorious Celebration, Emmanuel Mabisa kuwa tutafute chumba cha kufanyia kazi zetu za graphics na kazi ya Mungu. Tulibahatika kupata maeneo ya Afrikasana sinza hapa Dar es Sallam. Tukajadili ni jina gani tutatumia, ndipo tulipokuja na jina la RUMATZ tukimaanisha RU ni Rulea, MA ni Mabisa na TZ ni Tanzania. Tukaamua kuboresha tovuti yetu iliyoitwa www.rumatz.com ambayo ilikuwa ikiweka habari za Mungu. Ilifanya vizuri sana. Wakati tumeanzisha ofisi yetu ya RUMATZ mimi nilikuwa bado nafanya kazi na yule mzungu Ulric katika kampuni yake ya Roots-Markting Communication iliyoko Masaki.

Emmanuel Mabisa kiongozi wa Glorious Celebration kwa sasa

Nikiwa katika kampuni Mungu akaniwezesha kifedha na kuamua kutafuta eneo la kuishi, nilibahatika kupata chumba na sebule maeneo ya Lion Sinza. Nikaweza kulipa kodi ambayo ilikuwa ni 150,000 na unalipa kwa mwezi. Mungu aliniwezesha nikalipa kodi ya mwaka. Nikaa mwaka mmoja Mungu akanishangaza na kunibariki kupata gari, kwa kweli namshangaa sana Mungu!!!.

Kama unavyojua mwanadamu ana haki ya kuwa na mke au mwanamke kuwa na mume, nilimtafuta yule nimpendae ambaye sitataja jina lake na tukakubaliana kuwa tutaoana. Mpenzi wangu niliyempata hakuwa na ile hofu ya mUngu lakini alikuwa muumini wa kanisa fulani.  Nilimweleza mpenzi wangu amtumikie Mungu, alinikubalia na tukawa wapenzi na tukitegemea kuwa mume na mke hapo baadae. Baada ya mwaka kuisha shetani akaingilia kati na kuvuruga mahusiano yetu. Namshukuru Mungu mpaka sasa yule dada anaendelea na Mungu na Mungu amembariki sana kimaisha. Nilijifunza mengi kutoka kwake na kugundua kuwa ukimtumikia Mungu atakuondoa kutoka zero na kuwa milionea.
Ulipofika mwaka 2011, Mungu akaamua kuitimiza ndoto yangu ya kuwa mjasiliamali. Mungu akaanza kuniondoa taratibu kutoka katika hali ya kuajiliwa na kuwa mjasiliamali. Uongozi uliamua kunihamisha katika kitengo cha Graphics na kuwa  PR Asssitant wa kampuni ya simu ya Tigo nikiwa katika kampuni mama ya Roots iliyoitwa The Works. Niligungua kuwa Mungu akataka nijifunze jambo fulani fualni kuhusiana na maswala Public Relation ili inisaidia baadae.
Nikiwa mkoa wa Singida na Mkuu wa Mkoa, akinipongeza kwa kufikisha vitabu vya wanafunzi vilivyotolewa na kampuni ya Tigo.
Mungu akanishangaza tena kwa kunipa uwezo wa kununua kiwanja cha eka moja Pwani katika kijiji cha Mwanzo Mgumu. Ndugu yangu nayasema haya kwako kukuonyesha kuwa Mungu anaweza kufanya makubwa kama utamtumikia. Nilimshangaa sana Mungu kwa upendo wake. Na bei niliyoambiwa ilikuwa kiasi kidogo sana. Rafiki kama nimekukwaza kwa heli naomba unisamehe, lengo langu ni kumpongeza Mungu wangu na kumshukuru kwa yale ameyafanya kwangu.


Hapa ni Pwani Mwanzo Mgumu, na lile ndilo gari ambalo Mungu alipatia


Na hili ndilo shamba langu kuanzia kwa huyu dada mpaka kule niliko
Mwaka 2011 mwezi wa 11 ndipo nilipoacha kazi na kuwa full mjasiliamali. Maisha yakabadilika tena na kuwa magumu, kwani nilikuwa nategemea mshahara na sasa hakuna cha mshahara na hakuna mtu wa kunisidia. Kaka yangu ambaye alikuwa ananisaidia na aliyenisomesha, Amir Sanga akafariki. Nilichanganyikiwa lakini nilimtegemea sana Mungu.
Mungu akazidi kuniondoa katika hali ya kufanya kazi na mtu, ndipo akanitoa kufanya kazi na Emmanuel Mabisa na nikawa nafanya kazi zangu nyumbani. Nikaamua kutafuta jina lingine la kufanyia biashara kwani lile la RUMATZ akawa anatumia rafiki yangu Mabisa. Nafikiri ni Mungu aliyenipa jina la  RUMAFRICA. Nikatengeneza blogu ambayo ndio hii www.rumaafrica.blogspot.com ambayo inahusika na usambazaji wa Habari Njema za Mungu. Na baadae niliamua kuanzisha blogu nyingine ambayo inahusika na kazi zangu za graphics, inayoitwa www.rumaafricajobs.blogspot.com. Mungu akawa ananipa wateja na maisha yakawa yanasonga.

Nikiwa nyumbani akaja rafiki yangu Jackson aliyependa nifanye naye kazi katika kampuni yake ya Africhina. Nilimkatalia sana, kwani niliona yeye kama anataka kuvunja kusudi langu na malengo yangu. Alinibembeleza sana na kunishauri kuwa tutakuwa Partners katika kampuni yake. Baada ya kuona kuwa angependa tuwe Partners, nilimkubali na tukatafuta jina la kanpuni na kuiita AFRICHINA & RUMAFRICA. Rafiki yangu alikuwa amejijenga sana nikimaanisha alikuwa na kila kitu kinachohusika na maswala ya graphics na printing.Sikufurahia sana na utendaji wa kazi nikiwa mahali pale kwani niliona ndoto zangu zinapotea, na sioni ninachofanya. Nilikumbuka nilikotoka na nikaangalia nilipo na mbele yangu nikaona kuna njia nzuri ya mimi kwenda.

Siku moja nikiwa nyumbani kwangu Sinza kwa Remy, Mwezi Aprili 2012 mida ya saa nne usiku nikapigiwa simu kutoka Nigeria kwa simu  Nabii TB Joshua kuwa agependa mimi niende Nigeria nikaonane naye. Na hii ilitoka na kuvutiwa na blogu yangu niliyoitengeneza  na kuweka habari zake nyingi. Kwangu ulikuwa ni muujiza mkubwa sana, kwani sikutegemea katika maisha yangu kuwa nitaitwa na mtumishi wa Mungu ambaye ni tishio ulimwenguni. Nilifikiri katika dunia hii watu ni wangapi na kunitafuta mimi niliye wahi kuwa ombaomba miaka ya 2002. Nilikubaliana naye na  siku ilifika ya kukwea pipa hadi SCOAN na kuonana naye uso kwa uso na kushika mkono.
Nikiwa Ethiopia baada ya ndege kurudi tokea cameroon. Upande wa kushoto ni ile Engine iliyokuwa inavuja oil

Tukiwa safarini, tukiwa kwenye ndege maeneo ya Cameroon, ndege yetu ikawa inataka kudondoka kwani Engine moja ilikuwa inavuja oil, tukatangaziwa kuwa hali ni mbaya na hivyo tunajitahidi kujaribu kuigeza kuelekea Ethiopia. Ulikuwa ni wakati mgumi sana kwa maana ndege ilikuwa ikishuka chini kwa kasi. Mungu alitutetea tukafanikiwa kufika Ethiopia na kuunganishiwa ndege nyingine.
Tukiwa Cameroon wakati ndege inayumba
Niliporudi Tanzania kutoka Nigeria nikafanya na Jackson kwa muda  wa miezi kadhaa na kuamua kuachana naye. Nikarudi tena maisha ya kufanyia kazi nyumbani. Ndugu yangu usiombe, ujasiliamali unahitaji uvumilivu sana, nilitaabika sana.

Nikamshangaa tena Mungu wangu, maisha yalianza kubadilika na kuwa mazuri ukifananisha na nyuma kutokana na baraka kutoka kwa Nabii TB Joshua na wachungaji wangu wa hapa nyumbani. Kuanzia hapo niaamua kuwa mjasiliamali na ninamshangaa Mungu akanipa pesa na nikaweza kulipa hata pango la ofisi yangu ambayo inaitwa RUMAFRICA iliyoko Afrikasana Sinza Dar es Salaam.


Nikiwa ndani ya Sinagogi ya Nabii TB Joshua Nigeria
Mwezi wa Juni 2012 nikapatwa na jaribu lingine, ambapo mama yangu mzazi alifariki katika hospitali ya Chimala Mbeya. Ulikkuwa wakati mgumu sana kwangu, rafiki zangu wa jirani ambao nilitegemea watakuwa faraja kwangu wakanikimbia na kushindwa hata kufika nyumbani kunipa pole kwa kufiwa. Na hii hali ilikwenda hata kanisani kwangu ambako nako sikuona muumini yoyote kufika na kunifariji pale nyumbani kwangu. Nayasema haya kwa kusikitika sana, lakini natumaini yatakuwa somo kwa wengine. Nilijiuliza maswali mengi kama mwanadamu na kushindwa kupata majibu. Nikawa napata faraja kutoka kwa Mungu na kusahau yale machungu ya kufiwa na mama yangu. Nilishangaa kuona watu ambao sikuwa nao kivile katika kazi zangu za kidunia na za kiroho wakiwa msaada mkubwa sana kipindi namuuguza mama yangu na hata alipofariki, sitawasahau watu kama Mama Kevi Mwanza, Rosemary, Rose, Kemmy, Lister, Erick Brighton, Fred Msungu, Hellen kutoka Finland, Emmanuel Mabisa, Alex Kisonga, na wengine wachache ambao nimewasahau, walikuwa marafiki wangu wa karibu wakati mama amefariki.

nikielekea Mbeya kumuuguza Mama yangu, Ambangile Sanga

Nikimwangalia mama yangu, siku ya mwisho kwai siku iliyofuata akawa ananiaga

Na hapa juzi juzi nimepatwa na jaribu kubwa sana, naona umeshasoma katika shuhuda yangu ya hapo chini. Singependa kukueleza kwa sasa, ipo siku tutaongea.

USHAURI WANGU:

MOJA: Jaribu kuwa wewe na usiige maisha ya mwingine, utaumia

MBILI: Usimtegemee Mwanadamu, ila Mungu atakutumia wanadamu kukubariki

TATU: Acha woga na amini unachokifanya kuwa kitaleta mafanikio makubwa.

NNE: Simamia maono yako na usikubali yavunjwa na mtu yeyote yule.

TANO: Amini unakichokifanya, kuwa ni bora kuliko cha mtu mwingine.

SITA: Penda kuwa mtu unayeachilia yale ambayo yamekukwaza.

SABA: Heshimu kazi yako hata kama haiingizi kiasi unachotegemea

NANE: Omba sana kwa Mungu na kufanya yale Mungu anataka ufanye kwa kupitia masomo yaliyoko katika Biblia.

TISA: Usitegemee sana kuwa katika shida yako muumini au mtu fulani atakusaidia, simama katika maombi na kusema
Mungu akusaidie akupe watu ambao ni sahihi katika shida zako.

KUMI: Waheshimi wanakuheshimu na wasamehe wanakukosea.

KUMI NA MOJA: Uwe mtu wa toba kwani kuna mengi tunamkosea Mungu kwa kujua au kutojua.

KUMI NA MBILI: Waheshimu ndugu zako, wachungaji wako na watumishi wa Mungu hata kama watakukwaza, kwani nao ni wanadamu, ipo siku watapotea katika ulimwengu huu. Na tambua na wewe iko siku utakufa, jiweke safi na kuwa mtu wa msamaha.
-----------------------------------------

Ofisi yangu inajihusisha na maswala ya Graphics, Website na Blogs, Uuzaji wa Tshirts.
kama ungependa kufanyiwa kazi kama hizi:
Business cards, Brochure, Banner, Branding, Books, Flyers, Poster, Billboards, Cards, ID, Lightbox, Wheelcover, CD Cover, stickers, n.k

Pia tunapiga picha kwa kiwango cha juu sana!!!

Kama ungependa tangazo lako liwe katika blogu yetu, wewe wasiliana nasi na kama una jambo lolote kuhusu Mungu na ungependa tuliweke katika blogu yangu, nitumie na mimi nitaliweka

Karibu RUMAFRICA
Simu +255 715 851523
B/Pepe: rumatz2011@yahoo.com

WATASHINDANA LAKINI HAWATASHINDA KWA JINA LA YESU

Ushuhuda wangu ufanye kitu katika maisha yako.

AMENI










Comments

Unknown said…
Ahsante sana kwa kutuelezea historia ya maisha yako kwa kweli Mungu anakupenda sana. Unapokuwa karibu na Mungu, na shetani nae hachezei mbali, lakini sisi watoto wa Yesu daima tunaamini kwamba pale unapoona mitihani imezidi kuwa mingi na migumu, milango ya baraka nayo iko karibu kufunguliwa kutokana na imani yako kwa Mungu ilivyo. Nina imani kwamba Bwana Mungu ana makusudi na wewe katika maisha yako na kwamba endelea kumtumainia na hatokuacha kama alivyotuambia katika Jeremiah:33:3: "call to me and i will answer you andtell you great and unsearchable things you do not know". God bless you my brother and keep up the faith and the good job you are doing. Amen.