RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

SIWEZI KULUMBANA NA MAASKOFU


WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi imesema haiwezi kulumbana na maaskofu kufuatia kauli zao kuwa Serikali haijachukua hatua za maana kudhibiti vikundi vya kihalifu ambavyo vinatumia jina la waumini wa Dini ya Kiislamu kuchochea vurugu za kidini nchini.
Akizungumza na Mwananchi jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dk Emmanuel Nchimbi alisema hawezi kulumbana na maaskofu kwani hatua zinachukuliwa ikiwa ni pamoja na baadhi ya viongozi wa makundi hayo kuwa na kesi mahakamani.
Kauli hiyo ya Nchimbi inafuatia kauli ya Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa aliyoitoa wakati wa kufungua mkutano mkuu wa kanisa hilo mjini Bagamoyo hivi karibuni.
Katika hotuba yake hiyo ya ufunguzi, Malasusa alisema Serikali ina kigugumizi katika kusema ukweli kuhusiana na ghasia hizo na zingine zinazotokana na imani za kidini nchini na kudai kuwa Serikali haikupaswa kuishia tu kuwakamata watuhumiwa bali pia kufuta vikundi vyao.
Kuanzia katikati ya Oktoba mwaka huu, kulizuka ghasia katika Mji wa Zanzibar na Dar es Salaam vilivyokwenda sambamba na kuchoma makanisa.
Malasusa katika mkutano huo alitadharisha na kuitaka Serikali ipige marufuku vikundi hivyo  hata kama ni ndani ya kanisa analoliongoza.
Hata hivyo, kesi bado ziko mahakamani kwa viongozi wa wafuasi hao ambao kwa Zanzibar ni Farid Hadi Ahmed na Dar es Salaam, Sheikh Ponda Issa Ponda.
Mwenyekiti wa Jumuia ya Kikristu Tanzania (CCT), Dk. Peter Kitula ilidai kuwa ukimya wa Serikali katika kuzuia kashfa, uchochezi, matusi na uchokonozi mwingine wa wazi dhidi ya waumini wa dini ya kikristu kunaonyesha wazi kuwa serikali ina mkono wake.
“Jambo hili la maaskofu mnallikuza bure, wangapi wapo mahakamani” alihoji Nchimbi na kuongeza kuwa suala hilo lisikuzwe kwani linaweza kuwa na athari mbaya.

Comments