RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

KANISA LA MORAVIAN KWENYE HATIHATI YA KUFUNGIWA



Waziri wa Mambo ya Ndani, Matthias Chikawe ©Mwananchi

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe ametishia kulifuta Kanisa la Moravian kutokana na migogoro ya mara kwa mara inayolikumba.

Chikawe pia ametangaza kuyafutia usajili madhehebu na makanisa mengine yenye migogoro ya ndani, hali inayohatarisha amani ya nchi.

Waziri Chikawe alisema hayo jana wakati wa maombezi maalumu ya kuliombea taifa yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Karismatiki Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Alisema Kanisa la Moravian limekuwa katika migogoro kiasi cha waumini wake kupigana hadharani tena kanisani wakati wa ibada.

“Ninawataka viongozi wa kanisa hili kumaliza tofauti zao kupitia mabaraza yao ya ndani badala ya kufikishana katika vituo vya polisi, vinginevyo nitachukua hatua za kuyafuta kwa kuwa yanahatarisha amani ya nchi,” alisema na kuongeza:

“Moja ya majukumu ya wizara yangu ni pamoja na kusajili madhehebu na vikundi vya kidini chini ya Sheria ya Vyama Sura 337. Sitasita kuyafutia usajili madhehebu yoyote yanayotawaliwa na migogoro ili kuepusha shari.”

Chikawe aliwataka viongozi kuwa mfano wa kuigwa kwa kutumia fursa walizonazo kuwakumbusha waumini wao kuwa na hofu ya Mungu, pia kujenga umoja, amani na mshikamano miongoni mwao.

“Niwatake viongozi wa Kanisa la Moravian nchini kumaliza mgogoro wao kwa busara na kwa kutumia vitabu vya Mungu badala ya kupishana katika vituo vya polisi wakishtakiana,” alisema.

Kauli ya Chikawe inakuja ikiwa ni siku chache baada ya Askofu Kiongozi wa Kanisa la Moravian Tanzania, Alinikisa Cheyo kusema migogoro iliyolikumba kanisa lake inachangiwa na utovu wa nidhamu pamoja na kutojua taratibu za uongozi ndani ya kanisa.

Akizungumza mjini Mbeya, Makao Makuu ya kanisa hilo, Cheyo alisema utovu wa nidhamu unaambatana na ubinafsi na kutaka kufanya kazi kwa manufaa binafsi. Hivi karibuni, waumini na wachungaji wa Jimbo la Kusini Magharibi walifunga kwa makufuli na minyororo, ofisi ya askofu huyo Mtaa wa Jakaranda, Mbeya, wakimshinikiza ajiuzulu. Waumini hao walidai kuwa Askofu huyo amemfukuza Mwenyekiti wa jimbo hilo, Nosigwe Buya bila kufuata taratibu.

Mbali ya tukio hilo la hivi karibuni, kanisa hilo limekuwa na migogoro ya mara kwa mara mkoani Dar es Salaam katika mazingira tofauti. Pia limekuwa katika migogoro mingi ya uongozi tangu mwaka 2012, baada ya kuondolewa nyadhifa na kusimamishwa kazi kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Jimbo la Misheni ya Mashariki, Clement Fumbo.

Chanzo: Mwananchi

Comments