RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

MKWARUZANO MDOGO WATOKEA KANISANI KATIKA YA MAINDA NA MUUMINI MWENZAKE

Tunatambua ya kuwa sio binadamu yuko sawa kwa kila jambo, kuna wakati mtu anawezakukukwaza hata kama ameokoka na wewe ukakwazika na kumjibu vingine kabisa. Ruth Suka ‘Mainda’ anadaiwa kugombana na muumini mwenzake kwenye kanisa analoabudu kwa sasa, Amani limedokezwa.

TUJIUNGE NA MTOA HABARI
Kwa mujibu wa chanzo makini, tukio hilo la aina yake lilijiri kwenye kanisa hilo la kiroho lililopo chini ya mchungaji wake aliyetajwa kwa jina moja la Mwamposa, Sinza-Lion jijini Dar, Jumapili iliyopita.
Mtu mmoja aliyedai anaabudu kwenye kanisa hilo linalokuja juu kwa sasa, akizungumza Jumapili usiku kwa simu ya chumba cha habari cha Global Publishers, alisema Mainda alitofautiana na mwenzake (jina halikupatikana mara moja) wakati wakifanya usafi kama sehemu ya huduma yao kanisani hapo. “Jamani niwape habari, leo hapa kwenye kanisa la Mchungaji Mwamposa, Sinza-Lion, Mainda amegombana na muumini mwenzake kisa kikiwa ni kiti tu.
“Mainda alikuwa akisafisha viti ili aviingize kwa mchungaji huyo, mwenzake akaja na kukalia. Akaja juu, yule naye akaja juu! Acha wagombane,” alisema mtu huyo.

AMANI MZIGONI
Baada ya kudakishwa madai hayo, Amani liliingia mzigoni ili kupata undani ambapo mambo yalikuwa hivi; JUMATATU, SAA 4:00 ASUBUHI Kwa kuwa tukio lilidaiwa kujiri Jumapili, Jumatatu saa 4:00 asubuhi, mwanahabari wetu alifika kanisani hapo na kufanya ‘ushushushu’ kabla ya kujitambulisha kuwa anatoka Global Publishers.


Ruth Suka ‘Mainda’ akipozi. MUUMINI

Akielezea tukio hilo kwa undani zaidi, mmoja wa waumini ambaye hakutaka kutaja jina lake alidai tukio hilo lilitokea jana yake (Jumapili) wakati watumishi hao wakifanya usafi wa kawaida. Alidai kuwa, Mainda alikuwa akifuta vumbi kwenye viti ili aviingize kwa mchungaji, mara mwenzake akaja na kukalia kimojawapo na ndipo wakaanza kurushiana maneno.

“Wao ndiyo watenda kazi humu ndani, sasa unakuta labda mtu anamuagiza mwenzake amletee kitu fulani lakini anakataa. “Ninavyojua mimi ni kwamba, Mainda alikuwa akifuta viti na kuvipeleka ndani kwa mchungaji, mara mwenzake akaja na kukaa pale, wakaanza kuzozana: Lete kiti...wee unaona mimi nafuta ili viingie kwa mchungaji, wewe unakuja kukalia,” alisema mtumishi huyo akichukuliwa (kurekodiwa) sauti kwa sharti la kutotajwa popote.

MUUMINI MWINGINE
Muumini mwigine aliyekuwa eneo hilo naye alidakia huku akirekodiwa: “Ni kweli waligombana lakini baadaye waliwekwa chini na kumaliza tofauti zao na wote wanaendelea kutoa huduma kama kawaida. Watu wa Mungu hawawekeani visasi hata siku moja.”

MZEE MUUMINI
Baada ya kupata maelezo hayo, gazeti hili lilimfuata mzee mmoja aliyekuwa kanisani hapo muda huo ambaye hakutaka kutaja jina lake ambapo alikiri kuwepo kwa ugomvi wa Mainda na mwenzake huku akisisitiza kisa kilianza kwenye kiti. Alisema baadaye walisuluhishwa na wakapatana mambo mengine yakaendelea kwa amani. “Jamani hata hili jambo dogo limewafikia hadi ninyi? Hii sasa ni hatari! Waligombana kweli lakini waliwekwa sawa wakapatana.Kisa ni kiti tu, Mainda kakifuta ili akiingize kwa mchungaji mwenzake akaja kukikalia, hilo ndiyo tatizo,” alisema mzee huyo bila kutaja nafasi yake ya huduma katika kanisa hilo. Akaendelea: ”Kukwaruzana ni jambo la kawaida katika sehemu yenye mkusanyiko wa watu kama hapa, hasa kwa wasichana kama hawa.” Mwanahabari wetu alipotaka kuzungumza na Mchungaji Mwamposa kama anajua lolote juu ya sakata hilo, aliambiwa kiongozi huyo yupo safirini kwa huduma ya kiroho.

MAINDA HEWANI
Baada ya kutoka kwenye kanisa hilo, mwandishi wetu alimtwangia simu Mainda ambapo alipopatikana alisema: “Siyo kweli. Mimi sijui chochote. Kama unataka uje kanisani uongee na wachungaji.” Baada ya kukata simu na kupita dakika kadhaa, Mainda alipiga simu kwa mwanahabari wetu na kutaka kumjua ni nani aliyezifikisha habari hizo Global Publishers. Alijibiwa si maadili ya kazi kutaja chanzo cha habari.

JUMATATU SAA 10:00 JIONI
Siku hiyohiyo, mishale ya saa 10:00 jioni, gazeti hili lilirudi tena kanisani hapo ili kuzungumza na wachungaji kama alivyotaka Mainda ambapo lilibahatika kukutana na muumini aliyesema yeye ni mzee wa kanisa lakini akagoma kutaja jina lake.
Mzee huyo alisema hajui lolote na kwamba kama ni kugombana kwa watu kupo lakini kuhusu Mainda hakutaka kuzungumzia lolote. Kwa bahati nzuri, muda huo Mchungaji Mwamposa ambaye ndiyo alikuwa amerejea kutoka safarini alikuwepo, Hata hivyo, alikataa kuzungumza chochote kwa kuwa hakuwepo. “Mimi sikuwepo hivyo siwezi kuongea chochote maana sijaambiwa chochote,” alisema Mwamposa.

MUUMINI AHOFIA
Wakati mwandishi wetu anatoka nje ya kanisa hilo, alimuuma sikio muumini mmoja akimtaka amtajie jina la muumini aliyegombana na Mainda, lakini akasema: “Wewe ni mwandishi wa habari! Akha! Kama unataka huduma ya kiroho nitakusaidia lakini si hayo mengine, naogopa mwaya.”

KAMA ZALI, MAINDA HUYU!
Baada ya kumsikia muumini huyo, mzee wa kanisa na baba mchungaji, kama zali ghafla Mainda alitokea ambapo kwa upande wake, alikanusha tena madai hayo na kusema kuwa haelewi chochote kuhusiana na ugomvi huo. “Nashangaa kusikia hivyo na sijui chochote kuhusu hilo, kawaulize vizuri haohao waliokwambia,” aliwaka Mainda.

MNYONGE MNYONGENI, HAKI YAKE...
Pamoja na yote lakini Mainda anakuwa msanii nyota Tanzania ambaye amedumu katika mazingira ya kumtumikia Mungu tangu akate shauri la kuokoka takribani miaka miwili iliyopita. Amekuwa mstari wa mbele kuusimamia wokovu wake kwa dhati, akihudumu kanisani hapo kwa kufanya usafi asubuhi na jioni bila kukosa ibada.

Comments