RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

CLINTON ATEULIWA RASMI KUWA MGOMBEA WA CHAMA CHA DEMOCRAT

Kwa mara ya kwanza katika historia ya Marekani mwanamke amearifishwa na moja ya vyama viku vya nchi hiyo kuwania kiti cha urais.

Katika siku ya pili ya kikao chake kilichofanyika Jumanne huko mjini Philadelphia katika jimbo la Pennsylvania, kongamano la kitaifa la chama cha Democrat lilimteua Hillary Rodham Clinton, mama wa taifa wa zamani, seneta wa zamani wa jimbo la New York na waziri wa mambo ya nje wa zamani wa Marekani kuwa mgombea wa mwisho wa chama hicho katika uchaguzi wa rais wa Marekani ambao umepangwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu. 

Baada ya kufanyika sherehe za kukubali ugombea huo hapo  Alhamisi, Clinton ataingia rasmi katika mchuano wa kuwania kiti cha rais wa Marekani na mpinzani wake wa chama cha Republican Doland Trump.
Hillary Clinton baada ya kuteuliwa na chama chake kuwania kiti cha rais wa Marekani huko Philadelphia

Ili kumshinda mpinzani wake huyo, Clinton anategemea pakubwa umashuhuri wake wa kisiasa na uungaji mkono wa serikali iliyoko madarakani hivi sasa ambayo ni ya chama cha Democrat. 

Vilevile kuwa kwake mwanamke na sera zake za marekebisho ya kiuchumi na kijamii ni silaha nyingine inayotumiwa na timu yake ya kampeni za uchaguzi ili kumshinda Donald Trump. 

Hillary Clinton anatazamia kuwatisha wasomi na kambi za wapiga kura za wachache nchini humo kuhusiana na matamshi ya chuki ya Trump dhidi yao ili kupata fursa ya kuwa mwanamke wa kwanza katika historia ya Marekani kuketi kwenye kiti cha rais wa nchi hiyo. 

Hillary Clinton amekuwa akikimezea mate kiti hicho tokea mumewe alipokuwa rais wa nchi hiyo. 
Miaka minane iliyopita pia Clinto alikaribia kukichukua kiti hicho kabla ya Barack Obama rais wa hivi sasa wa Marekani kudhihiri ghafla na kumnyima fursa ya kuketi kwenye kiti hicho, sehemu ambayo alikuwa mama wa taifa kwa muda wa miaka minane.
Trump na Clinton kuchuana vikali katika uchaguzi wa kuwania urais Marekani

Hata hivyo inaonekana kuwa njia ya Clinton ya kurejea Ikulu ya White House si laini. Katika baadhi ya chunguzi za maoni zilizofanywa hivi karibuni, Trump ameonekana akiwa mbele ya Clinton kwa uungaji mkono wa kuingia White House. 

Katika siku ya kujiuzulu rasmi Bernie Sanders mpinzani wa Clinton katika chama cha Democrat hapo siku ya Jumanne katika kongamano la kitaifa la chama hicho mjini Philadelphia, Trump aliahidi kufanya juhudi za kuwashawishi wapiga kura wote waliokuwa wakimuunga mkono mgomea huyo wa chama cha Democrat wampigie kura yeye. 

Hata hivyo muungano wa mrengo wa kushoto wa chama cha Democrat una wasiwasi mkubwa kuhusiana na mitazamo ya kibaguzi na ya chuki dhidi ya wageni ya mwanasiasa huyo mtatanishi. Pamoja na hali hiyo lakini ni wazi kuwa hasira dhidi ya Clinton katika kipindi cha utawala wa Wademocrat na hasa katika mrengo wa Waliberali inazidi kuongezeka. Clinton amewasilishwa kama mgombea wa chama tawala katika hali ambayo Wamarekani waliowengi wanataka kufanyike mabadiliko ya kimsingi ya kiuongozi ili kutatua migogoro ya kisiasa na kijamii ya nchi hiyo.
Bernie Sanders

Waliberali wanaopigania mageuzi walikuwa wakimuunga mkono Sanders na kutumai kwamba ufichuliwaji wa kashfa ya baruapepe za Clinton ungemuwezesha mgombea wao huyo kumshinda Clinton katika uteuzi wa mwisho wa Kongamano la kitaifa la chama cha Democrat. 

Hata hivyo mwishowe Bernie Sanders amelazimika kujiondoa kwenye uchaguzi wa kuwania urais wa Marekani na kumuunga mkono Clinton ili kuzuia mgawanyiko kwenye chama na hatari kubwa zaidi yaani ya kutoa mwanya wa ushindi kwa Trump. 

Hata hivyo hakuna ushahidi wa kutosha unaothibitisha wazi kuwa waungaji mkono wote wa Sanders watampigia kura Clinton katika uchaguzi wa tarehe 8 Novemba. Kwa msingi huo tunaweza kusema kuwa kura milioni 13 za Sanders zitagawanywa kati ya Clinton, Trump na vyama vingine vinavyoshiriki katika uchaguzi huo. 

Uwezekano huo ukiandamana na kashfa kubwa za kisiasa kama vile za kusambazwa baruapepe na nara za kuvutia za Trump zikiwemo za 'tuifanye tena Marekani kuwa nchi yenye nguvu na uwezo mkubwa', ni mambo ambayo huenda yakaweka vizuizi katika njia ya Hillary Clinton kufikia ndoto yake ya miaka mingi ya kuwa rais wa kwanza mwanamke katika historia ya Marekani.