RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

RAIS MAGUFULI AWAAPISHA MAKAMISHINA/MANAIBU WA POLISI IKULU

Rais Dkt. John Pombe Magufuli alikuwa Ikulu akiwaapisha Manaibu Kamishna wa Polisi(DCP) na Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi(SACP) wapatao 58 kati ya 60 waliopandishwa vyeo hivi karibuni. Katika mambo yote Rais amegusia suala la maslahi kwa jeshi la polisi,rushwa na nidhamu katika utumishi.

Akiongelea Rushwa, Rais JPM anasema Jeshi la Polisi lijiepushe sana na vitendo vya rushwa vinavyolikosesha heshima katika jamii,anasema hivi karibuni amepata taarifa za rushwa kubwa ndani ya jeshi la polisi inayokadiliwa kuwa kati ya bilioni 40 hadi bilioni 60 ambazo zilipaswa kununua sare za jeshi la polisi lakini hakuna hata sare moja iliyonunuliwa,na wakati huohuo kuna magari karibu 70 ya jeshi la polisi yapo bandarini na hayakakombolewa,hivyo katoa maagizo uchunguzi wa haraka ufanyike na sehemu ya pesa hiyo ikalipie magari hayo haraka na yatoke bandarini.

Rais pia ameagiza jeshi la Polisi kuondoa utaratibu wa kuwaondoa Raia wote ambao ni watumishi wa jeshi la polisi na kuweka nafasi hizo kwa Polisi walio na taaluma hiyo,na kama hawana wataalamu basi waajiri watu ambao ni wataalamu wa fani hizo ambao watakuwa ni Polisi ndani ya jeshi na si raia,Anasema inashangaza moja ya wizi uliogundulika ni wa muhasibu mkuu wa Polisi ambaye ana tuhuma za ubadhirifu wakati ni raia ndani ya Jeshi,kiasi kwamba Polisi wanakimbizana na wezi wa kuku mtaani wanaacha wezi wa mabilioni walio ndani ya makao makuu ya Jeshi la Tanzania.

JPM pia anasema hakuna umuhimu wa kitu kinaitwa Polisi Jamii,anasema huwezi kuwa polisi ndani ya Maji ziwani unamkamata jambazi anateka wavuvi halafu unaanza kujadiliana nae wakati una bunduki na pisto,”Unajadiliana nini na jambazi?” Alihoji Rais JPM…dawa ya huyo ni kumlaza tu chini,huwezi kuwa Polisi halafu unachekacheka na muhalifu na huku una bunduki mkononi.Rais anasema hizo bunduki wanapewa kwa ajili ya kuzitumia,maana inafikia polisi hadi anapokwa silaha na jambazi kisa polisi jamii.Rais anasema inatakiwa ifike sehemu mtu akimuona Polisi aanze kuogopa,hayo mambo ya Polisi jamii ndio yanaongeza uhalifu,hakuna urafiki wa Polisi na Raia

Rais anasema kuna wakati watu walivamia kituo cha Polisi Chato,wakachoma moto na kuiba silaha,halafu mkuu wa kituo ana bastora kiunoni na bunduki,anabaki kusema “Polisi Jamii”,hakuna kitu kama hicho,wale watu wote waliokuja kuchoma kituo ilibidi “walazwe chini”.Hata kama yeye akikutwa ndugu yake “amelazwa chini” kwa tukio kama hilo basi atawapongeza polisi,maana hiyo ndio kazi yao na lazima kuwe na heshima kati ya polisi na raia.Wakuu wa Polisi wasiwasumbue askari wa chini wanapotumia nafasi zao “kuwalaza watu chini” hasa pale wanapokuwa wanaliletea mchezo jeshi la Polisi.

Ameviomba vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama kukaa pamoja na kushirikiana,ameagiza Polisi kuendelea kumsaidia kukusanya mapato kwa kuongeza ulinzi bandarini,kwani ni baora akawa na makontena machache yenye kulipa kodi kuliko kuwa na lundo lisilolipa kodi.

Rais anasema huko Sinza amepewa taarifa nyumba zinabaki tupu na watu wanakimbia,anasema na bado…maana watu walizoea kupangia “michepuko” upande mzima,unakuta mtu ana “michepuko” mitatu au zaidi na kila mmoja kampangia upande,weekend anaenda Dubai kwa shopping,hizo zote zilikuwa hela za wizi wizi.Sasa hakuna pesa ya bure,lazima watu wafanye kazi.

Mwisho Rais kawaasa polisi kuepuka kupendeleana,hata kama gari la RPC limevunja sheria za barabaranu ni kulikamata na kuchukua hatua.Akachombeza kidogo “Unakuta traffic police anapewa shilingi 5000 njiani ya kubrash viatu kwa kushinda juani na kwenye mvua watu wanasema rushwa,wakati kuna watu wanaiba mabilioni ya pesa.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Naibu Makamishna wa Polisi (DCP) na Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi (SACP) na Viongozi mbalimbali wa Serikali mara baada ya Makamishna hao kula Kiapo cha Uaminifu kwa Viongozi wa Umma Ikulu jijini Dar es salaam leo.Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Magufuli amewataka wasimamie utekelezaji wa Sheria bila woga na kuahidi kuboresha maslahi ya Jeshi la Polisi nchini.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Serikali mara baada ya Naibu Makamishna wa Polisi (DCP) na Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi (SACP, Ikulu jijini Dar es salaam.



Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Jaji Mstaafu Salome Kaganda akiwaongoza Naibu Makamishna wa Polisi (DCP) 35 na Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi (SACP) 23 kula Kiapo cha Uaminifu kwa Viongozi wa Umma mara baada ya kupandishwa vyeo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo Ikulu jijini Dar es salaam.



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora Mhe. Angellah Kairuki (kushoto) akizungumza jambo na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Eng. John William Herbert Kijazi (wa pili kutoka kushoto) Ikulu jijini Dar es salaam mara baada ya Naibu Makamishna wa Polisi (DCP) na Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi (SACP) kula kiapo cha Uaminifu kwa Viongozi wa Umma.Wengine ni Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Jaji Mstaafu Salome Kaganda na Inspekta Jenerali wa Polisi Ernest Mangu.



Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira (wa pili kutoka kushoto)akizungumza jambo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) George Masaju (kushoto) leo Ikulu jijini Dar es salaam mara baada ya Naibu Makamishna wa Polisi (DCP) na Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi (SACP) kula kiapo cha Uaminifu kwa Viongozi wa Umma.Wengine kulia ni Waziri na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Kulia) na Mhe. Hamad Masauni.



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Serikali mara baada ya Naibu Makamishna wa Polisi (DCP) na Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi (SACP) kula Kiapo cha Uaminifu kwa Viongozi wa Umma Ikulu jijini Dar es salaam leo.Kutoka kushoto ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) George Masaju,Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Meja Jenerali Projest Rwegasira (wa pili kutoka kushoto), Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Hamad Masauni, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba, Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora Mhe. Angellah Kairuki (kushoto), Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Jaji Mstaafu Salome Kaganda na Inspekta Jenerali wa Polisi Ernest Mangu.


Naibu Makamishna wa Polisi (DCP) na Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi (SACP) wakila Kiapo cha Uaminifu kwa Viongozi wa Umma mara baada ya kupandishwa vyeo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo Ikulu jijini Dar es salaam.

Naibu Makamishna wa Polisi (DCP) na Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi (SACP) wakifuatilia kwa Makini hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli mara baada ya kula Kiapo cha Uaminifu kwa Viongozi wa Umma leo Ikulu jijini Dar es salaam.


Rais Magufuli akihutubia.



RaisMagufuli akisalimiana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Ernest Mangu.