RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

MANENO ALIYOYASEMA RAIS MAGUFULI AKIWA NCHINI KENYA OCTOBER 31 2016


Rais Magufuli ambaye yuko nchini Kenya kwa ziara ya kiserikali ya siku mbili ambapo kabla ya Mkutano na waandishi wa habari leo October 31 2016 amepokelewa rasmi kwa kupigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride rasmi lililoandaliwa kwa heshima yake na baadaye kufanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta.


Rais Magufuli akizungumza na waandishi wa habari Ikulu ya Nairobi nchini Kenya amesema Kenya ni nchi inayoongoza kwa uwekezaji nchini Tanzania ikilinganishwa na nchi nyingine za Bara la Afrika ambapo amebainisha kuwa takwimu za kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC) zinaonesha kuwa Kenya ina jumla ya kampuni 529 zinazoendesha shughuli zake nchini Tanzania ambapo zimewekeza Dola za Marekani Bilioni 1.7 na zimeajiri watu 56,260.

Aidha Rais Magufuli amebainisha kuwa biashara kati ya Tanzania na Kenya imeongezeka kutoka Shilingi za Kitanzania Bilioni 652.9 hadi Shilingi za Kitanzania Trilioni 2.044.

>>>’Naomba niwahakikishie kuwa uhusiano na ushirikiano wetu ni mzuri na utaendelea kuwa mzuri zaidi, na kwetu sisi Tanzania, Kenya ndio nchi ya kwanza kwa uwekezaji kuliko nchi zote za Afrika’;-Rais Magufuli.

>>>’Tunashirikiana vizuri katika uchumi, watu wetu wanafanya kazi pamoja, yapo makabila yetu ambayo yanaingiliana kwa shughuli zao za kila siku na hata wanyamapori wetu wanazunguka katika nchi zote mbili bila kujali mipaka’;- Rais Magufuli.


Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Kenya, Uhuru Kenyatta amemshukuru Rais Magufuli kwa kukubali mwaliko wake na amemhakikishia kuwa Kenya itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano na Tanzania.

>>>’Kwetu sisi Tanzania ni ndugu zetu, ni kaka na dada zetu tunao ushirikiano wa siku nyingi na wa kidugu na tutahakikisha tunauendeleza ushirikiano na uhusiano huu mzuri ulioasisiwa na wazee wetu’;–Rais Kenyatta.

Rais Kenyatta amesema Tanzania na Kenya ni nchi zinazofanana kwa mambo mengi muhimu ikiwemo kubadilishana uongozi wa Serikali kwa njia ya amani na ameongeza kuwa katika mazungumzo yao wamekubaliana kuwa nchi hizi zitaendelea kuzisaidia nchi nyingine za Afrika Mashariki zinazokabiliwa na matatizo mbalimbali.

Aidha, Rais Kenyatta amesema Kenya itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi ya ushirikiano ikiwemo ujenzi wa miundombinu kama vile barabara ya Bagamoyo (Tanzania) hadi Malindi (Kenya) pamoja na mambo mengine ambayo Tume ya pamoja ya ushirikiano kati ya nchi hizi mbili (Joint Commission Cooperation) itayaainisha.