RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

MBUNGE LEMA ASAFIRISHWA KUTOKA DODOMA USIKU HADI ARUSHA, ASWEKWA MAHABUSU


Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema, amesafirishwa kutoka Mkoani Dodoma usiku wa kumkia jana na kuswekwa kwa mara nyingine tena Mahabusu Mkoani Arusha kwa mahojiano ya kutoa lugha za uchochezi.

Akizungumza leo na waandishi wa habari ofisini kwake , Kamanda wa Polisi Mkoani Arusha, Charles Mkumbo, amesema Lema wamemweka mahabusu mpaka watakapomaliza mahojiano.

Amesema kuwa endapo watamaliza mahojiano atafikishwa mahakamani wakati wowote, ili kujibu makosa anayokabiliwa nayo.

Mkumbo amesema Lema amekuwa akitoa maneno na lugha za uchochezi na kuzirudia kila mara, hivyo wameona vema wamweke ndani.

Amesema juzi walimkamata na kumuhoji, kisha kumwachia kwa dhamana, lakini kuna baadhi ya makosa hakuhojiwa, na ndiyo wanamuhoji.

Aidha licha ya kumkamata Lema na kuendelea kumuhoji, lakini hakutaja maneno yapi na lugha za uchochezi alizotoa Mbunge huyo.

Novemba Mosi mwaka huu, Kamanda Mkumbo akiwa anazungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, alitaja maneno ya uchochezi anayodaiwa Lema kutaja kuwa ni:

“Mheshimiwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania akiendelea kukandamiza demokrasia, siasa za ukandamizaji taifa litaingia katika umwagaji wa damu, nchi hii inaandaliwa kwenda katika utawala wa kidikteta,”