RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

NGOME YA WANAWAKE ACT YAMSHITAKI RC MAKONDA KWA KUMDHALILISHA AFISA ARDHI KINONDONI

Ngome ya Wanawake ACT Wazalendo imeitaka Tume ya Maadili na Utawala Bora kufanya uchunguzi na kuchukua hatua dhidi ya matamshi mbalimbali yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambayo yalikiuka sheria ya Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma wakati wa mkutano wake na wananchi eneo la Mabwepande juzi.

Ifuatayo ni taarifa waliyoitoa Ngome ya Wanawake ya Chama cha ACT-Wazalendo kutaka Mhe. Paul Makonda awajibishwe;

Ngome ya Wanawake ya Chama cha ACT-Wazalendo imeshtushwa na kuhuzunishwa na kauli zisizo za kiuongozi na zisizozingatia kanuni za Maadili ya Utumishi wa Umma zinazoendelea kutolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Jana (juzi Jumatatu), katika mkutano anaouita wa kutatua kero kwa wakazi wa Dar es Salaam, ndugu Makonda ametumia maneno ya kudhihaki, kudhalilisha, kukejeli na kutukana hadharani watumishi anaowasimamia, kitendo ambacho ni kinyume na maadili ya Watanzania.

Kitendo cha Mkuu wa Mkoa Makonda akiwa katika eneo la Mabwepande, Wilaya ya Kinondoni Mkoani Dar es Salaam kumtolea lugha ya udhalilishaji Afisa Ardhi wa Manispaa ya Kinondoni, Bi. Rehema Mwinuka kwa kumtamkia kuwa; “Hawa ndio vichaa tunaohangaika nao, toka hapa..” hakikubaliki na kimetusikitisha sana, na tunakilaani kwa nguvu zetu zote.


Kauli kama hii siyo tu haikupaswa kutolewa na kiongozi mkubwa katika ngazi ya Mkoa lakini pia ni kauli mbaya ambayo ililenga kumdhalilisha na kumvunjia heshima yake mbele ya umma Bi. Rehema Mwinuka.

Kutokana na udhalilishaji huo uliofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sisi Ngome ya Wanawake ya ACT Wazalendo, Leo Jumanne, Novemba 29, 2016 tumepeleka mashtaka rasmi dhidi ya Mkuu wa Mkoa huyo mbele ya Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya viongozi wa umma kuwataka wamuwajibishe kwa kitendo chake hicho cha utovu wa nidhamu na maadili ya utumishi wa umma.

Ngome ya Wanawake ACT Wazalendo inamtaka pia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam atambue kuwa kwa kuzingatia Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002 pamoja na Kanuni za Maadili ya Utumishi wa Umma, kanuni ya 65(1) inamtaka mtumishi wa umma;

“kuepuka kufanya vitendo viovu au kutamka maneno yanayolenga kuwaaibisha watumishi wa ngazi moja, za chini yao au wa vyeo vya juu”
Alichofanya Mkuu wa Mkoa ni kumuaibisha na kumtolea lugha ya udhalilishaji Bi Rehema Mwinuka kinyume cha Sheria na Kanuni za Utendaji katika Utumishi wa Umma.

Ngome ya Wanawake ACT Wazalendo inaitaka Tume ya Maadili na Utawala Bora ifanye uchunguzi na kuchukua hatua dhidi ya matamshi mbalimbali yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ambayo yalikiuka sheria ya Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma.

Ngome ya Wanawake ACT Wazalendo inayataka pia Mashirika na Asasi mbalimbali zinazosimamia Haki za Binaadamu, Haki za Jinsia na Utawala Bora kupaza sauti dhidi ya kauli isiyo ya kiuongozi iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa dhidi ya Afisa Ardhi wa Manispaa ya Kinondoni Bi Rehema Mwinuka.

Kadhalika, Ngome na Chama kwa ujumla tutaendelea kuwasemea wanyonge wote popote walipo kwa kadri ya uwezo wetu.

Esther Kyamba, 
Katibu, Ngome ya Wanawake – ACT Wazalendo.
Novemba 29, 2016