RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

MASWALI MATANO YA KUUAWA KWA MPELELEZI…


Polisi wa wakiwa eneo la tukio


PWANI: Taarifa kutoka Kibiti wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani zinasema, mpelelezi wa wilaya hiyo (OC-CID), SP Peter Kubezya ameuawa kwa kupigwa risasi ya tumboni na watu wanaosadikiwa kuwa ni wahalifu na kuacha maswali 5.

Sambamba na askari huyo, Rashid Mgamba ambaye ni Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (C CM), Peter James Kitundu ambaye ni afisa uvuvi wa wilaya hiyo, nao waliuawa katika mapambano hayo.

Tukio hilo lilijiri usiku wa saa 1, Jumanne kuamkia jana Jumatano ambapo watu sita wenye bunduki zinazosadikiwa kuwa ni aina ya Sub Machine Gun (SMG) walivamia Kituo cha Kutoza Ushuru wa Mazao ya Kilimo na Misitu Kijiji cha Jaribu Mpakani na kuwauwa kwa kuwapiga risasi, Mgamba na Kitundu na kuchoma moto eneo hilo.

Eneo la tukio huko Pwani

Wakati tukio likiendelea inadaiwa kuwa, Mpelezi wa Mkoa wa Pwani RCO, SSP Mbise na OC CID, Kubezya walifika eneo hilo baada ya kupigiwa simu na watu wanaodaiwa kuwa ni miongoni mwa wauaji hao.

Wakati mapigano yakiendelea, OC CID huyo alijeruhiwa kwa risasi tumboni na kufariki dunia wakati akipelekwa Hospitali ya Misheni ya Mchukwi iliyopo Kibiti kwa matibabu. Habari zinadai kuwa, baada ya tukio hilo, wahalifu hao walitelekeza pikipiki mbili walizozitumia kufika eneo la tukio na kutokomea gizani kwa miguu.

Pia wahalifu waliacha kipeperushi cha kupinga uwepo wa kizuizi cha kutoza ushuru katika eneo hilo wakieleza kuwa, kinalenga kuwadhulumu wananchi mali zao, hususan mkaa na kuwataka wananchi hao wachukuwe mkaa ambao baadhi yao walivamia na kuchukuwa. Hivi karibuni, Wilaya za Mkuranga na Rufiji zimekuwa zikikumbwa na mauaji ya watu kwa kutumia SMG.


Watu wanaodaiwa kuua wanatajwa na vyombo vya serikali kuwa ni wahalifu lakini wenyewe na wanavijiji wa maeneo hayo wamekuwa wakisema ni magaidi.

MASWALI MATANO TATA Wakizungumza na Amani jana, baadhi ya wanakijiji cha Jaribu Mpakani walisema watu hao ni wale waliowahi kutamka kuwa, wataua viongozi 18 wa vijiji maeneo hayo kutokana na kuwachoma kwa polisi kwamba, wao ni wahalifu.

SWALI LA KWANZA Je, ni kweli watu hao ni wale magaidi wanaoua viongozi katika maeneo hayo, kwamba walikuwa kwenye muendelezo wa mauaji yao?

SWALI LA PILI Je, askari mgambo na afisa uvuvi waliouawa ni miongoni mwa watu waliotajwa na watu wanaoua viongozi ili kufikia idadi ya watu 18?

SWALI LA TATU Inasemekana kuwa, watu hao waliacha kipeperushi cha kupinga utozwaji ushuru kwa wananchi wakisema unalenga kuwadhulumu watu wa eneo hilo. Je, inaweza kuwa sababu ya watu hao kuwatoa roho wenzao? Au kuna kingine kilichojificha?

SWALI LA NNE Kutokana na kuibuka kwa mauaji ya mara kwa mara maeneo hayo, je, Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani halina mpango wowote wa kuhakikisha wanafutilia mbali watu hao?


SWALI LA TANO Wauji hao wamekuwa wakitumia silaha aina ya SMG, ambazo kisheria zinamilikiwa na serikali na ni silaha zenye sifa za kivita. Je, watu hao wanazitoa wapi silaha hizo? Si miongoni mwa zile bunduki zilizowahi kuibwa kwenye vituo mbalimbali vya polisi nchini mwaka 2015?

RPC PWANI ANASEMAJE? Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, ACP Boneventura Mushongi jana hakupatikana kuzungumzia tukio hilo ambapo simu yake ya mkononi iliita muda mrefu bila kupokelewa