RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

Mwanamuziki Bobi Wine achaguliwa kuwa mbunge Uganda


Mwanamuziki mashuhuri wa mtindo wa Afrobeats nchini Uganda Ugandan Robert Kyagulanyi Ssentamu, maarufu kama Bobi Wine, ameshinda ubunge katika uchaguzi mdogo nchini humo.

Wine, ambaye aliwania kama mgombea huru, aliwashinda wagombea wengine wane katika eneo bunge la Kyadondo Mashariki katikati mwa Uganda.

Alipata kura 25,659 kutoka kwa kura 33,310 zilizopigwa, gazeti la serikali la New Vision limeripoti.

Gazeti hilo linasema baada ya kutangazwa mshindi, aliahidi kuangazia zaidi kuwaunganisha raia.

"Jambo langu la kwanza ninalotaka kufanya ni kufanikisha maridhiano kati ya viongozi wa Kyadondo Mashariki...Ninataka siasa zitulete pamoja... jinsi muziki ufanyavyo."

Mwanamuziki huyo alikuwa amekamatwa na polisi na kuhojiwa kwa muda kabla ya kuachiliwa siku chache zilizopita.

Kiti hicho cha ubunge kiliachwa wazi baada ya mahakama kuamua kuwa uchaguzi uliofanyika mapema mwaka jana haukufuata kanuni na sheria za uchaguzi.

Kiongozi wa chama cha upinzani cha FDC Kizza Besigye amempongeza mwanamuziki huyo kwenye Twitter.

Ameandika: „Ushindi mkubwa kwa Mheshimiwa Bobi Wine. Hongera - Nguvu za Raia!! Ndio maana watu wa Wakiso hawakuruhusiwa kupiga kura mwaka 2016."

Wine alianza muziki mapema miaka ya 2000.

Baada ya uchaguzi mkuu wa 2016, alichomoa wimbo kwa jina Situka, ambao maana yake ni Inuka au Zinduka kwa Kiluganda.

Kwenye wimbo huo, anatoa wito kwa raia wa Uganda kuchangia katika vita dhidi ya rushwa na ukiukaji wa haki nchini mwao.