MelK Premium Suits

TANGAZO MUHIMU

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

BISHOP DR. M.E. ADMIN

BISHOP DR. M.E. ADMIN

SANDLANDS HOTEL KARIAKOO

BABA ADAIWA KUTAKA KUMTOA KAFARA MWANAYE!

Msichana anayedaiwa kupewa mimba na Babu mmoja.


STORI: IMELDA MTEMA, DAR
DUNIA imekwisha! Ndivyo unavyoweza kusema kufuatia kuwepo kwa matukio mawili ya kusikitisha, moja la baba aliyefahamika kwa jina la Ombani Emmanuel mkazi wa Pansiansi jijini Mwanza, kukamatwa na polisi kwa kumfanyia vitendo vya kikatili mwanaye ikiwa ni pamoja na kudaiwa kutaka kumtoa kafara na tukio lingine ni la babu mmoja kudaiwa kumpa mimba mjukuu wake.

Katika tukio la kwanza imedaiwa kuwa Emmanuel, hivi karibuni alikamatwa na polisi kwa kile kinachodaiwa kumfanyia mambo ya ajabu mwanaye mwenye umri wa miaka 10, huku majirani wakidai kuwa, kulikuwa na kila dalili za baba huyo kutaka kumtoa kafara.…Akiwa katika pozi.

Akizungumza na gazeti hili, Mkurugenzi wa Taasisi ya Nitetee, Flora Lauo alidai mambo aliyokuwa akifanya baba huyo yalikuwa yakiwakera majirani wengi kwa sababu mbali na kuwepo kwa dalili za kutaka kumfanyia tukio baya, pia alikuwa hamruhusu kujichanganya na mtu yeyote hata kucheza na wenzake.

HILI LA KAFARA
Kwa mujibu wa Flora, baadhi ya majirani wanaoishi karibu na baba huyo walikuwa wakihofia baada ya kutomuona mtoto huyo nje huku baba yake akionekana kila mara akiwa na kisu kikubwa.

“Hili la kutaka kumtoa mwanaye kafara ni madai tu ya majirani kutokana na mazingira wanayoyaona pale nyumbani, lakini kubwa ni kutompa haki zake za msingi sambamba na hilo la kumfungia ndani,” alisema Flora.

KUOGA NI MARA MOJA KWA WIKI

Baadhi ya majirani walidai kuwa baba huyo alikuwa akimfungia ndani mtoto wake na kumruhusu kuoga mara moja kwa wiki na ni Jumapili tu.

“Huyu baba ni zaidi ya maajabu, huwa tunamuona mtoto akimruhusu kuoga mara moja tu kwa wiki, yaani Jumapili tu na humfungia ndani na kujisaidia humohumo,” alidai mmoja wa mashuhuda.

Mtoto hasomi

Mashuhuda hao waliendelea kuanika kuwa baba huyo alimuachisha mtoto shule kisha akawa anamsomesha Biblia kila siku na akiambiwa ampeleke shule anadai eti akifanya hivyo atakutana na mashetani hivyo ni bora akae nyumbani.

Alipoulizwa na majirani kuwa kitendo cha kumfungia ndani kutwa nzima anajisaidia wapi, alisema kuwa chumba anachoishi amechimba kishimo kidogo kwa ajili ya kujisaidia haja ndogo huku haja kubwa wakijisaidia kwenye maboksi kisha kwenda kutupa kwenye makaburi.

MKE AMKIMBIA

Habari kutoka kwa majirani zinasema mke wa bwana huyo aliyezaa naye mtoto huyo, amekimbia nyumba siku nyingi kutokana na vituko alivyokuwa akifanyiwa.

Majirani hao walidai kuwa baba huyo aliwahi kutoa sadaka kwa kufanya kafara ya mbuzi ambaye alimchinja na kumuweka ndani huku akimchoma kidogokidogo bila kumla akidai ni sadaka.

Walidai alianza tena kufunga kwa siku 14 na akawaambia kuwa zikiisha atatoa kafara kwa Mungu kutokana na mafundisho kwamba Mungu alisema toa sadaka kitu unachokipenda.

“Tulipoona amenunua sime kwa ajili ya kazi hiyo ya kafara ikiwa ni siku ya 10 baada ya kufunga tuliamua kwenda kumripoti polisi.

“Tulifanya hivyo kwa sababu tulikuwa tukimsikia akisali na kumuomba Mungu kuwa yupo tayari kumtolea sadaka, ndipo tulipopata hofu kwamba asije akawa anataka kumtoa kafara mwanaye ndipo tukalifikisha suala hili polisi.

ATIWA MBARONI

Baada ya majirani kusikia maombi hayo waliamua kutoa taarifa kwenye Taasisi ya Nitetee iliyoamua kwenda Kituo cha Polisi Pasiansi ambao walifika na kumchukua baba huyo na sime iliyokuwa imenolewa na kumuweka mahabusu huku wakimfungulia jadala la mashitaka lenye namba MZN/RB/7296/2017 la Julai 21, mwaka huu.

Polisi waliamua kumnyang’anya mtoto na kukabidhiwa Taasisi ya Nitetee na Mkurugenzi wake Flora Lauo amethibitisha kumpeleka mzazi huyo polisi na kukabidhiwa mtoto huyo ili amlee.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, DCP Ahmed Msangi hakupatikana jana lakini afisa mmoja wa polisi aliyeomba hifadhi ya jina lake alikiri kukamatwa kwa Emmanuel kwa upelelezi zaidi.

HILI LA BABU KUMPA MIMBA MJUKUU

Wahenga walisema; Ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni! Wakati hilo la baba kudaiwa kumfanyia vitendo vya ajabu mwanaye, babu mwenye umri unaokadiriwa kuwa ni miaka 65, aliyejulikana kwa jina moja la Nyaganga anadaiwa kumpachika mimba mjukuu wake (jina linahifadhiwa kwa sababu za kimaadili) ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili.

Akizungumza bila uoga, mtoto huyo ambaye ujauzito wake ni wa miezi saba, alidai alikuwa akiishi na baba yake Tarime mkoani Mara kabla ya kufikwa na mazito hayo.

“Babu yangu alinichukua nikiwa na umri wa miaka sita nikaenda kuishi naye Nyasaka, mkoani Mwanza, babu huyo akawa ananifanyisha mchezo mbaya,” alisema.

Mtoto huyo aliendelea kudai kuwa babu huyo aliendelea kumfanyia mchezo huo huku akimpa vitisho kuwa akisema kwa baba yake atamwambia asimuendeleze na shule hivyo alikuwa akivumilia mpaka akazoea.

Mtoto huyo aliendelea kudai kuwa babu huyo alikuwa akimfanyia vitendo hivyo wakati bibi yake akiwa ameondoka kwani huwa anaondoka alfajiri kwenda kuuza nyanya sokoni.

“Mnaweza kunilaumu kwamba kwa nini nilikubali lakini alikuwa akinipa vitisho, nikawa nimezoea hadi nilipokuja kunasa ujauzito,” alidai binti huyo.

Msichana huyo aliendelea kudai kuwa wakati bado hajajigundua kama ni mjamzito, walimu ndiyo walianza kumtilia shaka na kumpeleka mpaka Kituo cha Polisi cha Nyasaka, ambapo walimpima na kumgundua ni mjamzito.

Kufuatia hatua, babu huyo alifunguliwa jalada la kesi lenye namba MZN/RB/4553/017 KUBAKA na mtoto huyo alichukuliwa na kwenda kulelewa kwenye Taasisi ya Nitetee ya jijini Mwanza huku taratibu za kesi zikiendelea.

Hata hivyo, inadaiwa kuwa, baada ya babu huyo kutaitiwa na polisi alijitetea kuwa, anasumbuliwa na ugonjwa wa henia, hivyo hawezi kufanya mapenzi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, DCP Ahmed Msangi hakupatikana kuzungumzia kesi hiyo, lakini afisa mmoja wa upelelezi ambaye siyo msemaji alithibitisha kuripotiwa tukio hilo na kwamba upelelezi unaendelea.
0