RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

DKT MWANJELWA AISHAURI (IITA) KUONGEZA SPIDI UTOAJI ELIMU KWA WANANCHI KUKABILIANA NA SUMU KUVU





Na Mathias Canal, Geita
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Mary Mwanjelwa ameishauri Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Kilimo ukanda wa Kitropiki (IITA) kuongeza kasi ya utoaji elimu kwa wakulima nchini kuhusu kadhia ya Sumu Kuvu.

Alisema kuwa elimu hiyo inatakiwa kutolewa katika maeneo mbalimbali nchini ili wananchi waweze kutambua namna bora katika uandaaji wa mashamba wakati wa msimu wa kilimo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mashamba hayashambuliwi na magugu wala wadudu waharibifu.

Naibu Waziri ametoa ushauri huo wakati akizungumza na Msaidizi wa Mawasiliano wa Utafiti katika Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo ukanda wa Kitropiki (IITA) nchini TanzaniaBi Eveline Massam mara baada ya kutembelea Banda hilo wakati wa Maonesho ya 36 ya siku ya Chakula Duniani ambayo Kitaifa yanafanyika Katika Uwanja wa CCM Kalangalala Mjini Geita kuanzi Octoba 10 mpaka Octoba 16.

Dkt Mwanjelwa alisema kuwa wakulima wengi nchini wanalima pasina kufahamu taratibu za kilimo cha kisasa jambo ambalo linapelekea mazao yao kuathiriwa na wadudu husani Sumu Kuvu na kupelekea uduni wa mavuno.

Alisema kuwa endapo Taasisi hiyo ya (IITA) itaongeza nguvu ya utoaji elimu kwa wakulima kwa kushirikiana na wataalamu wa Wizara ya kilimo, wananchi watanufaika na kilimo chao ikiwa ni pamoja na kuwa na mavuno mengi.

Alisema Sumu Kuvu inahatarisha afya za watumiaji wa mazao mbalimbali ya chakula na biashara, kwani chakula na malisho ya mifugo iliyo athiriwa na sumu kuvu hupunguza uzalishaji huku mazao yenye kiwango kikubwa cha Sumu Kuvu zaidi ya kiwango kinachoruhusiwa kutekelezwa au yanauzwa kwa bei ya chini.

Aidha, zipo athari za moja kwa moja kwani endapo binadamu au mnyama atakula chakula chenye malisho yenye kiwango kikubwa cha Sumu Kuvu anaweza kupoteza maisha.

Kwa upande wake Msaidizi wa Mawasiliano wa Utafiti katika Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo ukanda wa Kitropiki (IITA) nchini Tanzania Bi Eveline Massam alisema kuwa Sumu Kuvu huzalishwa wakati fangasi aina ya Aspergillus anaposhambulia mbegu shambani/ghalani.

Aliongeza kuwa Ukuaji wa fangasi na athari za sumu kuvu husababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa (Ukame wa ongezeko la joto), Mbinu duni za kilimo kabla na baada ya kuvuna mazao kwa mfano; ukaushaji hafifu wa mazao punde yanapovunwa, na uhifadhi duni wa mazao ghalani na wadudu waharibifu.

Sumu Kuvu ni aina za kemikali za sumu zinazozalishwa na aina ya Ukungu au Fangasi wanaoota kwenye mbegu za nafaka kama vile mahindi, mbegu za mafuta kama karanga, jamii ya kunde na pia mazao ya mizizi. Pia sumu Kuvu hupatikana katika bidhaa za mifugo kama vile maziwa, mayai na nyama pale ambapo chakula kinacholiwa na mifugo kitakuwa kimechafuliwa na sumu hizo.

Sambamba na hayo pia Naibu waziri wa Kilimo Mhe Dkt Mary Mwanjelwa alitembelea Banda la Benki ya Maendeleo ya kilimo, Banda la Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe, Banda la Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe na Banda la Mamlaka ya chakula na dawa (TFDA).

Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani hufanyika kila mwaka kuanzia Octoba 10 mpaka Octoba 16 ambapo kwa mara kwanza yalianza mwaka 1981. Hivyo maadhimisho ya mwaka huu ni ya 36 na yanasherehekewa kwa pamoja na maadhimisho ya miaka 72 ya kuanzishwa kwa FAO tarehe 16 Oktoba, 1945.


Comments