RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

KADJANITO: CHRISTIAN BELLA ALINISHAWISHI NIACHE GOSPEL





Khadija Said Maige ‘Kadjanito’


UKIRUDI nyuma miaka sita kisha ukaulizia miongoni mwa wasanii wa kike waliokuwa wakitisa kwenye Muziki wa Bongo Fleva ni wazi utatajiwa wengi kutoka Jumba la Kuibua Vipaji (THT) ambao ni Mwasitti, Linah, Recho Kizunguzungu pamoja na Kadjanito.

Maumivu Niache ni wimbo uliomtoa Kadjanito katika Bongo Fleva na kujipatia umaarufu kisha zikafuatiwa nyimbo mfululizo ambazo nazo zilitikisa kama vile Si Ulisema, One More Night na Sina Maringo.

Maisha yanakwenda kasi sana! Baada ya kuimba Bongo Fleva, Kadjanito ambaye jina alilopewa na wazazi wake ni Khadija Said Maige aliamua kuachana na muziki huo na kujiingiza kwenye Muziki wa Injili ‘Gospel’.

Mashabiki wengi hawakuamini kutokana na uwezo mkubwa wa kucheza na sauti wa Kadjanito lakini kitendo cha kuamua kubadili dini kutoka Uislamu na kuwa Mkristo kisha kufunga ndoa ya Kikristo na Tresor Lisimo kiliuaminisha umma kuwa amefanya alichokidhamiria.



Kwa sasa hajulikani tena kama Khadija Said Maige wala Kadjanito, jina alilobatizwa baada ya kuwa Mkristo ni Natasha Lisimo na ndilo analotambulika kama msanii wa nyimbo za Injili akiwa tayari na nyimbo kadhaa ambazo ni Nifanye Nini na Ufunguo Wangu ni Yesu aliomshirikisha Bahati Bukuku ambao pia unabeba jina la albamu yake ya kwanza.

Star Showbiz imepata bahati ya kukutana naye na kufanya naye ‘Exclusive interview’ na katika makala haya anafunguka mengi zaidi kuhusiana na maisha na muziki wake;

STAR SHOWBIZ: Mipango uliyonayo kwa Muziki wa Injili nje ya Tanzania ni ipi?

NATASHA: Sasa hivi naongozwa na Roho Mtakatifu, nafanya kazi kwa kujituma naamini Mungu atanionesha njia ya kwenda sehemu yoyote.

STAR SHOWBIZ: Unauonaje Muziki wa Injili?

NATASHA: Kiukweli nauona ni Neno (Chakula cha Kiroho) ambacho nashiba na kuwa binadamu niliyekamilika.

STAR SHOWBIZ: Ulishawahi kupiga bendi (Skylight Band) wakati unaimba Bongo Fleva, vipi una mpango wa kuwa na bendi ya Muziki wa Injili?

NATASHA: Ninayo hiyo ndoto, huwa namwambiaga hata mume wangu (Tresor) kwa sababu napenda sana muziki wa live, namuomba Mungu aniongoze nifanikiwe.

STAR SHOWBIZ: Ulishawahi kupata kishawishi cha kuurudia Muziki wa Bongo Fleva?

NATASHA: Nimeshawahi kushawishiwa sana tu na watu kurudia muziki huu tena wengine tulikuwa tukiimba wote Bongo Fleva kama vile Christian Bella ambaye aliniambia kuwa nikiimba naye nitatoka fasta lakini nikasema hapana, acha niendelee na Gospel.

STAR SHOWBIZ: Kuna msanii yeyote wa Bongo Fleva aliyetamani kuwa kama wewe akakufuata?

NATASHA: Wapo wengi sana wanatamani kuimba, nimekuwa nikiwaambia njooni, huku kuna amani.

STAR SHOWBIZ: Upoje na wazazi wako kwa sasa baada ya kupishana nao kauli kipindi unabadili dini na kuolewa Kikristo?

NATASHA: Unajua suala hili la wazazi ni la kumuachia Mungu kwani mwisho wa siku maisha yangu nimeamua kuyakabidhi kwa Mungu, naimani hata yale mabaya yote anaweza kuyabadilisha na kuwa mazuri. Uwezo wa Mungu ni mkubwa unazidi kutenda miujiza katika maisha yangu.

STAR SHOWBIZ: Mumeo anakusapoti vipi katika muziki wako?

NATASHA: Ni zawadi kutoka kwa Mungu, ananisapoti kila kona ya maisha yangu, nafikiri Mungu aliona huyu anaweza kila kitu. Siwezi kutunga nyimbo za Injili lakini yeye ndiye anayenitungia, anachukua maneno kwenye Biblia na kunishauri kuyatumia.

STAR SHOWBIZ: Ulishawahi kufikiria kuimba naye kwenye Muziki wa Injili?

NATASHA: Mume wangu ni mcheza mpira zaidi ya hapo ni muombaji, anaweza kukuombea ukapona lakini siyo muimbaji kabisaa.


STAR SHOWBIZ: Ukipata nafasi ya kukutana na JPM utamwambia nini juu ya muziki unaofanya?

NATASHA: Kwanza nitamshukuru Mungu kwa maana anaweza kunikutanisha na kila mtu, nitamwambia asapoti Muziki wa Injili, awe anatupa ile mialiko ya Ikulu, inapendeza sana watoto wa Mungu kuwa naye karibu kula naye chakula cha usiku, kuimba naye huko.

STAR SHOWBIZ: Ikitokea umeitwa kwenye shoo ya Bongo Fleva, upo tayari kupafomu?

NATASHA: Itategemea wananiita kuimba Bongo Fleva au Injili lakini kama ni Bongo Fleva siwezi kupafomu nyimbo hizo kwani nilishaachana nazo japokuwa hazikuwa mbaya.

STAR SHOWBIZ: Tumeona wasanii wengi wakijiingiza kwenye dini hawataki nyimbo zao walizokuwa wakiimba za kidunia kuendelea kupigwa, mfano Suma Lee pamoja na Mzee Yusuf, kwa upande wako vipi?

NATASHA: Siwezi kutoa kauli kama hiyo, maisha yangu ni ushuhuda, siwezi kuwakataza lakini kupitia nyimbo hizo watu wanaweza kujiuliza huyu mtu siku hizi yupo wapi ndipo wanapata kujifunza kumbe nimebadilika. Watu wanaweza kujiuliza; ‘kama kweli huyu mtu (Natasha) ameacha Bongo Fleva na kugeukia Injili kwa nini mimi?’

MAKALA: ANDREW CARLOS

Comments