RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

PAPA FRANCIS AMTEUA ASKOFU MKUU RUWAICHI KUMRITHI PENGO






Balozi wa Papa nchini, Askofu Mkuu Joseph Chenos (kulia) akiwa na aliyekuwa Askofu Mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo (kushoto) alipomsika Yuda Thaddaeus Rwaichi kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza katika viwanja vya vya Kawekamo jijini humo. (Picha na Maktaba).

BABA Mtakatifu Francis amemteua Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza Yuda Thaddeus Ruwaichi kuwa mrithi mtarajiwa wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, ambalo limekuwa linaongozwa na Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo. Kwa uteuzi huu, Askofu Mkuu Ruwaichi anakuwa Askofu Mkuu Mwandamizi Mwenye Haki ya Kurithi Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Padri Richard A. Mjigwa wa Vatican News ameandika katika mtandao wa Vatican, na Padri Raymond Saba, Katibu Mkuu wa Baraza la Maskofu Tanzania (TEC) ametoa taarifa rasmi kwa umma kuhusu uteuzi huo.

Inasemekana kuwa uteuzi huu maana yake huenda mchakato wa kustaafu kwa Kardinali Pengo umekamilika, hasa kutokana na matakwa ya kisheria kuhusu umri, na kwa sababu ya afya yake kutetereka.

Kabla ya kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Kardinali Pengo naye aliteuliwa kuwa askofu Mkuu Mwandamizi Mwenye Haki ya Kurithi tarehe 22 Januari 1990. Aliteuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam tarehe 22 Julai 1992 baada ya kustaafu kwa Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa.

Kabla ya uteuzi huu, Askofu Mkuu Ruwaichi alikuwa ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza tangu tarehe Novemba 10, 2010. Kwa uteuzi huu wa leo, Askofu Mkuu Ruwaichi amepitia katika mikono ya wateuzi watatu – Papa Yohanne Paulo II, Papa Benedicto XVI, na Papa Francis.

Askofu Mkuu Ruwaichi alizaliwa tarehe 30 Januari 1954, Mulo, Kilema, Jimbo Katoliki la Moshi. Alipadirishwa tarehe 25 Novemba 1981, akapewa daraja la uaskofu tarehe 9 Februari 1999. Baba Mtakatifu Yohane Paulo II alipomteua kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Mbulu, na akawekewa wakfu tarehe 16 Mei 1999.

Tarehe 15 Januari 2005, Baba Mtakatifu Yohane Paulo II akamteua kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Dodoma na kusimikwa rasmi tarehe 19 Februari 2005. Tarehe 10 Novemba 2010, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akamteua kuwa Askofu mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza, akasimikwa rasmi tarehe 9 Januari 2011. 


Comments