RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

DRC yaendelea kupata shinikizo kuwashirikisha wanasiasa wote katika Uchaguzi Mkuu


Rais wa DRC Joseph Kabila Kabange katika mkutano na waandishi wa habari, ikulu Kinshasa.REUTERS/Kenny Katombe


Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo CENCO, linataka wanasiasa wote kushirikishwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwezi Desemba na makubaliano ya kisiasa ya mwaka 2016 kuheshimiwa.


Wito huu umekuja, wakati huu wanasiasa mbalimbali wakiendelea kuwasilisha maombi ya kuwania urais, huku hatima ya mwanasiasa wa upinzani Moise Katumbi ikiwa haifahamiki baada ya kukwama nchini Zambia, baada ya kuzuiwa kuingia DRC na serikali.

Wakati huo huo, Umoja wa Afrika unataka haki za Wacongomani wote kuheshimiwa, wito ambao pia umetolewa na Umoja wa Ulaya.

Serikali ya DRC inaendelea kupata shinikizo kutoka Jumuiya ya kimataifa ili kufanikisha mchakato huu wa uchaguzi lakini pia kuhakikisha wanasiasa wote wanashiriki uchaguzi.

Hayo yanajiri wakati ambapo rais Joseph Kabila ambaye Katiba haimruhusu kuwania muhula wa tatu, anaendelea kusalia kimya wakati ambapo imesalia siku moja tu kabla ya kumalizika muda wa mwisho wa wagombea urais kuwasilisha fomu za kuwania uchaguzi mkuu ambao umepangwa kufanyika Desemba 23.

Siku ya Jumatatu muungano wa vyama vinavyoongozwa na Katumbi, Ensemble, viliandaa maandamano katika maeneo mbalimbali ya nchi, lakini maandamano hayo yalitawanywa na vikosi vya usalama, kwa mujibu wa shirika la habari la AFP.

"Tunataka Katumbi kurudi nchini Congo bila kuchelewa," waliandika waandamanaji hao kwenye mabango yaliyokua yakishikiliwa na wanawake ambao walikua miongoni mwa waandamanaji, kulingana na video iliyorushwa kwenye mitandao ya kijamii.

"Hadi wakati huu, hakuna sababu kwamba tunaweza kuahirisha tarehe ya mwisho kwa zoezi hili," Corneille Nangaa, Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ameliambia shirika la habari la AFP.

Siku ya Alhamisi na Ijumaa wiki jana rais Kabilaalizuru nchi jirani ya Angola, ambayo inafuatilia kwa karibu mchakato wa uchaguzi nchini DRC.

Hapo awali, aliwatuma Waziri wake wa Mambo ya Nje, mkuu wa Idara ya Upelelezi (ANR) na mkuu wa idara ya ujasusi katika nchi jirani ya Rwanda kukutana na rais Paul Kagame.

Comments